MWENYEKITI wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli amesema ushindi wa CCM wa ubunge na madiwani katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika juzi nchini ni ishara ya ushindi wa chama chake katika uchaguzi ujao kutokana na wananchi kuonesha imani kwake na serikali yake.
Rais Magufuli aliyasema hayo kwa waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kumpokea Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan aliyefika Ikulu, Dar es Salaam jana akiwa kwenye ziara yake ya siku mbili nchini.
Rais Magufuli alisema ushindi huo ni kipimo cha utendaji wake kwa wananchi na hivyo umemuongezea ari ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wake bila ya kujali changamoto mbalimbali zilizopo.
“CCM Oyee! Mnaonaje ushindi wa CCM? Hii inadhihirisha ni namna gani wananchi walivyo na imani na mimi na serikali yangu. Tumeshinda ushindi wa kishindo katika kata na Jimbo, wenyewe mmeshuhudia namna tulivyowapiga. Au mnasemaje?” Rais Magufuli aliwaambia waandishi wa habari na kisha akawashukuru na kuelekea eneo lake maalumu akimsubiria Rais wa Uturuki kwa ajili ya kumpokea.
CCM mbali ya kushinda kiti cha ubunge cha Dimani visiwani Zanzibar, imeshinda kata 18 kati ya kata 19 zilizofanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani juzi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kufa kwa waliokuwa wakishikilia nyadhifa hizo na kufutwa kwa matokeo kwa amri ya mahakama.
Kata ambazo CCM imeshinda ni Nyarenanyuki (Arumeru, Arusha), Isegehe (Kahama, Shinyanga), Nkome (Geita), Kiwanja cha Ndege (Manispaa Morogoro), Lembeni (Mwanga, Kilimanjaro), Ihumwa (Dodoma), Matevez (Meru, Arusha), Kimwani (Muleba, Kagera), Igombavanu (Iringa), Kijichi (Mbagala, Dar es Salaam), Ng’hambi (Dodoma), Kinampundu (Singida), Kasansa (Katavi), Malya na Kahumulo (Mwanza), Mkoma (Mara), Misugusugu (Kibaha, Pwani).
Aidha, CCM imeshindwa katika Kata ya Duru mkoani Manyara, ambako mgombea wa Chadema, Ali Shaaban ameibuka mshindi. Kwa upande wao, baadhi ya wasomi wamesema kwamba chama cha mapinduzi kimeshinda kutokana na kutekeleza ahadi za kuondoa kero za wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Francis Michael alisema kwamba wananchi wa kada za chini wanaiamini CCM kwa sasa hivi kwa kuwa Rais John Magufuli amejikita kushughulikia masuala yanayowakera.
Alitoa mfano kwamba kitendo cha serikali kuondoa kero ya kodi katika mazao mbalimbali yamefanya wananchi wengi hasa wakulima waiamini Serikali ya Awamu ya Tano.
Pia alisema kitendo cha kupata huduma ya uhakika katika taasisi za serikali hasa hospitali tofauti na miaka ya nyuma ni jambo ambalo pia limechangia chama hicho kipate ushindi katika maeneo mengi ambako Uchaguzi Mdogo ulifanyika.
Aliongeza kuwa licha ya kuwepo watu ambao wanalalamika kuwa fedha hazipatikani, wanaolalamika sio wananchi wa chini bali ni watumishi ambao walizoea kuchukua rushwa na sasa mirija hiyo imekatika.
Pia alisema fedha imekosekana kwa wapiga dili ambao nao hawana athari katika masuala ya kura. Alitoa mfano kitendo cha Rais Magufuli kuzuia wamachinga wasihamishwe maeneo wanakofanyia biashara badala yake waachwe au watafutiwe maeneo mbadala kwanza pia yamesaidia kuwapa matumaini wananchi wa kawaida ambao ndio wapiga kura.
“Mimi naona kama Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea na mwendo huu wa kushughulikia kero za wananchi sidhani kama wapinzani watafurukuta huko mbeleni,” alisema Dk Michael.
Naye Dk Eve Maria Semakafu alisema CCM imeshinda katika kata hizo kuliko vyama vya upinzani kwa sababu kata hizo nyingi zilikuwa zinaongozwa na CCM yenyewe na hivyo kushinda huko ni sawa na kurejesha kiti chao.
Pia alisema kata nyingi ambako CCM imeshinda ni vijijini ambako vyama vya upinzani havina mizizi na vingine havina ofisi jambo ambalo lifanya chama tawala kuwa na wafuasi wengi kuliko vyama vya upinzani.
Akizungumzia iweje CCM ishinde wakati maeneo mengi kuna njaa, Dk Semakafu alisema kwamba huko vijijini hakuna njaa bali maeneo ambayo yana kawaida ya ukame ndio upungufu wa chakula na sio kwa sababu ya Rais Magufuli.
Alisema maeneo ya Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Singida na Mara kwa miezi ya kama hii ni kawaida kuwa na ukame hivyo akasema kwamba jambo hilo haliwezi kuwafanya wananchi wakichukie chama tawala kwa sababu ni kawaida yao.
“Mimi nimefanya utafiti katika maeneo hayo kwa miaka mingi, nafahamu ukame wa maeneo hayo, hivyo suala la njaa ni kwa wanasiasa na sio kwa wananchi,” alisema.