Wafugaji wa Kimasai Kenya wadaiwa kuwajeruhi Watanzania

WANANCHI wa vijiji vya Kirongo Chini na Kiwanda, Wilaya ya Rombo wanaopakana na nchi jirani ya Kenya, wameingia katika mgogoro na wafugaji wa jamii ya Kimasai kutoka nchini Kenya na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa na kulazwa hospitali.

Wafugaji hao wanadaiwa kuwapiga na kuwajeruhi wakulima wa Tanzania, huku wengine wakiwakamata wananchi wa vijiji hivyo na kupelekwa kwenye vituo vya Polisi vya Wilaya ya Taveta.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Agness Hokororo, alithibitisha Wamasai hao waliingiza mifugo yao wiki iliyopita katika moja ya shamba la mkulima na baadaye kuwavamia, kuwashambulia na kuwasababishia majeraha.

“Ni kweli kuna wakulima wa kwetu walijeruhiwa na mmoja alishonwa nyuzi 14 na mwingine amelazwa hadi sasa Hospitali ya Rufani ya KCMC. Hata hivyo, tumeshakutana katika vikao vya ujirani mwema, kati ya Wilaya ya Taveta na Rombo na tukakubaliana kwamba mkulima au mfugaji atakayeingia kwa mwenzake akamatwe,” alisema.

Mashamba yanayodaiwa kuchungiwa mifugo na kusababisha mgogoro huo ni yale yaliyolimwa mahindi, alizeti, maharage, karanga, migomba na mihogo.

Kwa mujibu wa Hokororo, jana (juzi) Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Rombo (SSP), John Mtalima, alikwenda Kaunti ya Taveta nchini Kenya kufuatilia kama wafugaji hao wamekamatwa, kwa kuwa kulishafanyika utambuzi maalumu kwa wahusika ambao walitajwa kwa majina na wakazi wa Taveta.

Mmoja wa majeruhi hao, Protas Sianga, aliimbia Nipashe kuwa Wamasai hao walitokea nchini Kenya na kuingiza makundi makubwa ya mifugo kwa nguvu katika mashamba ya wakulima na kisha kulishia mazao yao.

“Walipokuja na hiyo mifugo tulijaribu kuwaondoa, lakini Wamasai hao wakaanza kutupiga kwa kutumia rungu na sime wakilazimisha kuchungia katika mashamba yetu, na kibaya zaidi wanawalazimisha wakulima kufyeka uzio wa katika mashamba yao ili waingize mifugo yao,” alisema Agatha Akwilini, mmoja wa majeruhi.

Mkazi wa kijiji cha Kiwanda Wilaya ya Rombo, Gervas Tarimo, alisema kama Serikali za Tanzania na Kenya hazitachukua hatua za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo, kuna uwezekano wa kulipuka kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji wa Kimasai toka Kenya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad