CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimepongeza jitihada za Serikali ya
Awamu ya Tano ya kuanza kulipa madeni ya walimu, lakini imekumbushia
deni lake linalofikia Sh trilioni 1.060 kutokana na malimbikizo ya
kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi Desemba mwaka jana.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa chama
hicho, Ezekiah Oluoch wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
madai ya walimu na upungufu wa walimu shuleni.
Oluoch alisema kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi Desemba mwaka
jana, katika mwaka wa fedha wa 2016/17 serikali imewalipa walimu 182,882
jumla ya Sh bilioni 124.6 sawa na asilimia 10.5 ya deni linalodaiwa
katika kipindi hicho.
Alisema CWT inapongeza jitihada hizo, japokuwa hazijakidhi matarajio ya walimu ya kulipwa kwa asilimia mia.
Akizungumzia deni hilo katika kipindi hicho, alisema limeendelea
kukua na kufikia Sh trilioni 1.06 sawa na asilimia 89.5 ya kiasi
kilichokuwa kinapaswa kulipwa ambacho hakijalipwa.
Akizungumzia mchanganuo wa madai ya walimu, Oluoch alisema mafao ya
walimu wastaafu 6,044 pamoja na tozo ni Sh 556,048,000,000, madeni
yasiyohusiana na mishahara zaidi ya walimu 150,000 wanadai jumla ya Sh
180,000,000,000.
Alisema madeni ya mishahara ya walimu waliopandishwa madaraja Januari
hadi Machi 2016, walimu 85,945 wanadai jumla ya Sh 301,374,312,000 na
kwamba deni hilo linaongezeka kila mwezi kwa kiwango cha Sh
25,114,526,000 kuanzia Januari hii hadi Juni, 2017 ambapo lisipolipwa
hadi Juni, 2017 kutakuwa na ongezeko la Sh 150,687,156,000 ambayo
haikuingizwa kwenye deni la hadi Desemba, 2016.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CWT alisema ni matumaini yao kuwa serikali
itachukua hatua za haraka, kuwalipa walimu madeni yao na kuwaajiri
walimu wote waliohitimu, badala ya kuwaacha mitaani ambapo wataajiriwa
wakiwa wamesahau mbinu za ufundishaji.
“Walimu wanajua kwamba fedha zipo, kinachotakiwa ni utashi wa Rais
John Magufuli. Akiamua hata leo, fedha zote za walimu zitalipwa hata
wiki hii,” alisema Oluoch.