WANASAYANSI wa Kituo cha Anga cha Marekani (NASA), wamegundua jiwe kubwa lenye utajiri wa kutisha wa madini ya aina mbalimbali linaloelea angani.
Thamani ya utajiri wa madini yaliyopo katika jiwe hilo, unaelezwa kuwa ni zaidi ya uchumi wa dunia nzima.
Kutokana na ugunduzi huo, NASA wanapanga kuruka maelfu ya kilomita angani mwaka 2023 kwenda kwenye jiwe hilo ambalo kama litafanikiwa kurudishwa duniani, linaweza kuleta utajiri wa kufuru.
Likiwa katikati ya Sayari ya Mars na Jupiter, jiwe hilo linaaminika ni kiini cha ndani cha moja ya sayari zilizokufa.
Kwa mujibu wa wanasayansi, jiwe hilo ni la kipekee na limeundwa kwa madini ya metali kwa asilimia 100.
Jiwe hilo lenye umbo la duara lina urefu wa kilomita 200 na lina madini kama chuma, nickel na wanasayansi wanasema upo uwezekano mkubwa wa kuwa na madini adimu duniani kama dhahabu, platinamu na cobalt.
Jiwe hilo ambalo ni sayari mfu, lina thamani ya fedha nyingi mno, chuma peke yake kilichopo katika jiwe hilo, kinaweza kuwa na thamani ya Dola za Marekani 10,000 quadrillion, hii ni kwa mujibu wa mchunguzi mkuu wa jiwe hilo, Profesa Lindy Elkins-Tanton.
Uchumi wa dunia kwa jumla hivi sasa una thamani ya dola za Marekani 73 trilioni.
“Kwa sasa, kwenda kwa NASA katika anga za juu kunaleta dhana halisi ya ugunduzi. Safari hiyo, itawezesha kufika katika sehemu yenye kitu ambacho hakijawahi kuonekana wala kujulikana. Itatoa nafasi kwa wanasayansi kuona kitu ambacho kilikuwa kinafikirika hadi kufikia hivi sasa.
“Bado hatujaweza kufahamu mambo mengi, lakini tunadhani jiwe hili ni kiini cha metali ya sayari ndogo iliyoharibiwa kutokana na nishati kubwa, mwendo kasi wa dunia,” anaeleza Elkins-Tanton
Mpango huo wa kufika katika anga lililopo jiwe hilo, unatarajiwa kuzinduliwa mwaka 2023 na hadi kufikia mwaka 2030 chombo cha anga za juu kitakuwa kimefika eneo lililopo.
Wanasayansi ambao wametumia muda mwingi kulichunguza jiwe hili wanasema ndiyo jiwe kubwa la metali kwenye mfumo wa jua lililopo umbali wa kilomita 300 na inaaminika kuwa na kiasi kikubwa chuma na nickel.
Jiwe hilo kwa mara ya kwanza aliliona mwanaanga wa Kitaliano Annibale de Gasparis mwaka 1852 na kupewa jina la mungu wa roho wa Kigiriki Cupid.
Mwanzoni, ilidhaniwa kuwa ni jiwe la barafu lakini miaka ya 1980 wanaanga walishangazwa kuona rada ikisoma kuwa jiwe hilo lilikuwa linaundwa na metali.
Wanasansi wanaamini kuwa, jiwe hilo limepoteza ganda lake la nje, kutokana na msuguano na msukumano ambao umefanyika kwa mamilioni ya miaka.
Ili kupata ukweli zaidi kuhusiana na ugunduzi ambao bado unaacha maswali mengi, NASA itapeleka chombo chake katika eneo lililopo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kisayansi ambao unatarajiwa kuchukua muda mrefu.
Hii ni nafasi ya ugunduzi wa aina mpya ya dunia ambayo haijawahi kuonekana, si mwamba wala jiwe la barafu bali ni metali tupu,” anasema Elkins-Tanton ambaye ni Profesa katika chuo Kikuu ha Arizona nchini Marekani.
Anaongeza: "Jiwe hili ni aina pekee ya umbo ambalo limeweza kugundulika kwenye mfumo wa jua, ni njia pekee ya binadamu kuona shehemu ya kiini cha sayari iliyokufa. Mara nyingi tumekuwa tukijifunza sehemu ya ndani au kiini kwa kutembelea na kutizama sehemu za juu.
Chombo kitakachokwenda katika anga lililopo jiwe hilo, kitachukua miaka saba kufika. Pia kitakaa kwenye jiwe hilo kwa miezi sita kikijaribu kurekodi vitu mbalimbali kama muonekano, usumaku na vitu vilivyomo ndani yake.
Mpango huo ni sehemu ya mpango wa ugunduzi wa NASA utakaogharimu dola za Marekani milioni 450 wenye lengo la kujifunza kuhusu mfumo wa jua miaka milioni 10 tangu kuzaliwa kwa jua.
Mpango wa pili utazinduliwa mwaka 2021 ambao utalenga kuchunguza mabaki ya maombo ambayo yapo jirani na sayari ya Jupiter.