Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein akikagua gwaride la vikosi mbalimbali vya kijeshi katika sherehe za mapinduzi, miaka iliyopita
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein, leo anatarajiwa kuwaongoza maelfu ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Sherehe za maadhimisho hayo ambazo mwaka huu zimeanza mapema zinafikia kilele hii leo katika uwanja wa amani visiwani humo huku ukitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali za pande zote mbili, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Pamoja na mambo mengi uwanjani hapo Rais Shein anatarajiwa kukagua gwaride maalum lilioandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo ya mapinduzi matukufu katika visiwa hivyo.
Kwa upande wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, yeye ataongoza wananchi wa Tanzania Bara katika maadhimisho hayo akiwa mjini Shinyanga kwa mkutano mkubwa wa hadhara unaofanyika katika uwanja wa Kambarage.
Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika Januari 12 mwaka 1964, yakiongozwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume.