WATUMISHI 10 wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Mbeya (Ifisi) waliotimuliwa kazi na Bodi ya hospitali hiyo kwa maelezo kuwa hawana sifa, wamezua sokomoko hospitalini hapo baada ya kuorodhesha majina ya zaidi ya watumishi 20 wakidai walinunua vyeti.
Watumishi hao walifikisha orodha hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, wakidai kuwa watumishi hao walifanyiwa mpango na baadhi ya viongozi wa hospitali hiyo kuwasaidia kununua vyeti hivyo.
Kwa mujibu wa watumishi hao, vyeti hivyo vilikuwa vinanunuliwa kwa Sh. 200,000 kutoka katika moja ya chuo cha uuguzi jijini hapa.
Mmoja wa watumishi hao walioondolewa hospitalini hapo, Subira Mwanjali, alithibitisha kwenye mkutano kati ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wa Kanisa la Uinjilisti ambao ni wabia wa hospitali hiyo, kuwa yeye ni miongoni mwa walioombwa fedha hizo kwa ajili ya kununuliwa cheti.
“Mimi ni miongoni mwa watu tulioambiwa tutoe Sh. 200,000 ili nikanunuliwe cheti, lakini nilikataa kwa sababu ninacho cheti changu halisi cha taaluma ya uuguzi. Walituondoa sisi na wakiwaacha watu ambao tunaamini hawana vyeti ila wamenunuliwa,” alidai Mwanjali.
Naye Anne Mwangindwa, alidai kuwa uongozi wa hospitali hiyo uliwaondoa kazini bila kufuata taratibu za kazi ikiwamo kutowalipa stahiki zao.
Alidai kwamba baada ya kuona hawatendewi haki, waliamua kupeleka malalamiko yao kwenye Chama cha Wafanyakazi wa Afya nchini (Tughe) ili wapate haki zao, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea.
“Sisi hatukatai kupunguzwa kazini, lakini tunachotaka ni kulipwa stahiki zetu kama zinavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria za kazi, wamekuwa wakituzungusha hivyo hatuna imani na hawa watu japo ni watu wa Kanisa,” alisema Mwangindwa.
Kwa upande wake, Esther Mwaswalwiba, ambaye yupo upande wa kundi la waliopunguzwa mishahara, alidai kuwa wamepunguzwa mishahara kutoka Sh. 320,000 mpaka 50,000, kiasi alichosema hakiwezi kuwasaidia kuendesha maisha yao.
Alisema kupunguza mishahara hiyo ni sehemu ya kutaka kuwatengenezea mazingira ya kufukuzwa kabisa kama wenzao walioondolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Mchungaji Tito Nduka, alikataa tuhuma zilizoelekezwa kwa uongozi wa hospitali hiyo kwa maelezo kuwa watumishi hao wameondolewa kutokana na agizo la Rais la kuwaondoa kazini watumishi wasio na vyeti.
Alisema watumishi hao waliondolewa na Bodi ya hospitali hiyo baada ya kubainika kuwa hawana vyeti vya kidato cha nne na hivyo hakuna uonevu wowote uliofanyika.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Makalla, aliunda timu ya watu wanane kuchunguza mambo makuu matatu yaliyotajwa kwenye malalamiko hayo.
Timu hiyo inaundwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, Xavery Mhywela, Maofisa Usalama wa Taifa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya na baadhi ya maofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa timu hiyo itafanya kazi ndani ya siku 10 na majibu yatakayofanya hatma ya watumishi hao ijulikane pamoja na waliotuhumiwa kuhusika.
Alikabidhi timu hiyo baadhi ya nyaraka ambazo watazitumia kwenye uchunguzi ikiwa ni pamoja na orodha ya watumishi 21 wanaodaiwa kununuliwa vyeti, majina ya watu 10 waliopunguzwa kazini pamoja na nyaraka zinazoonyesha stahiki zao.