Waziri TAMISEMI, Simbachawene Amtega Makonda, Ampa Siku 3 Kuwaondoa Machinga Katika Barabara za DART

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, George Simbachawene amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema kuwaondoa wamachinga wanaofanya biashara katika miundombinu ya barabara za mwendokasi (DART) ndani ya siku tatu kuanzia leo

Simbachawene amezitaka mamlaka ya Mkoa wa Dar es salaam, na Wilaya ya Ilala kuhakikisha kwamba wamachinga hawarudi katika maeneo hayo kwa namna yoyote ile na kwamba hilo likishindikana, viongozi husika watakuwa wameshindwa kazi

"Ninaagiza wamachinga waondoke katika miundombinu ya barabara za BRT, Rais John Magufuli alipoagiza wasibughuziwe hakumaanisha wakae eneo lisilostahili, au wawe wanakaa barabarani, alimaanisha wamachinga wastaarabu wanaofuata sheria na wala hakuwaagiza wavunje sheria na kukiuka haki za baadhi ya watu", alisema na kuongeza 

"Nikiona wamerudi, Mkuu wa Mkoa na Wilaya kazi itakuwa imewashinda". 

Aidha, amewataka wamachinga kuondoka kwa hiari yao na kwamba kama wakikaidi agizo hilo mamlaka husika zitawaondoa kwa nguvu

"Wengi wanakaa katika makutano ya barabara hasa maeneo ya Fire, Kariakoo na kituo kikuu cha Gerezani. Hali hii inahatarisha usalama wa waenda kwa miguu sababu wengi hunusurika kupata ajali", alisema 

Pia amesema wamachinga hao ni changamoto kwa usafiri wa mwendokasi

"Changamoto ya Dart ni wamachinga kufanya biashara katika barabara za DART. Hii suala halikubaliki kabisa na halivumiliki na tutatumia nguvu kuwaondoa", alisema 

Chanzo : Dewji blog
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad