Magari ni kati ya vitu vinaundwa kwa ubunifu mkubwa zaidi duniani, magari yamekuwa yakifanya dunia kuwa sehemu rahisi kufikika kwa haraka ingawa ni kwa maeneo yenye barabara tu. Magari sio tena hitaji la wanaume pekee, hata wanawake wanamiliki magari mazuri na ya kisasa kila siku.
Leo nimekutafutia hii taarifa kuhusu vitu vya kujua kwenye magari; vipo vingi kuanzia kwenye aina ya gari unalotaka kununua, uimara wake, kampuni inayotengeneza n.k; nyingi zimekuwepo tangu zamani sana, na zimekuwa zikishindana kila siku kuunda magari ya kisasa.
Nimekukusanyia hapa leo kampuni 10 zilizotajwa kuwa bora zaidi kwenye kuunda magari ya kisasa duniani.
10. BMW
Inawezekana ulikuwa haufahamu nini kirefu cha herufi hizi tatu “BMW”, hii inasimama badala ya maneno “Bavarian Motors Work”kampuni ya kuunda magari iliyoanzishwa mwaka 1916 na waanzilishi wake ni marafiki watatu Franz Jozef Popp, Karl Rapp,na Camillo Castiglino; kutoka nchini Ujerumani, BMW haikuanza kama kampuni ya kuunda magari, ilikuwa ikizalisha Injini za ndege.
Baadaye ikaanza kuunda magari na pikipiki zenye speed kubwa. Sasa hivi, magari yanayoundwa na BMW yamekuwa yakitajwa kuwa kati ya magari ya starehe na imara duniani.
9. Mercedes-Benz
Mercedes-Benz pia ni kampuni ya kuunda magari kutoka Ujerumani na ilianzishwa mwaka 1926 na marafiki wawili ambao niGottlieb Daimler pamoja na Karl Benz. Inafahamika sana kwa kuunda magari ya kisasa na starehe, magazi ya mizigo, na mabasi ya abiria. Mercedes-Benz ni kampuni inayounda magari yenye uwezo kugundua kitu kinachosogea karibu yake wakati wa usiku, jambo linalofanya dereva kujiupusha na ajali.
Mbali na sifa za Mercedes-Benz kuwa moja kati ya makampuni yanayounda magari ya kisasa duniani, pia ina sifa ya kuunda magari yanayotajwa kuwa na usalama zaidi kwa watumiaji wake.
8. Audi
Hapa tena ni aina ya gari ya Kijerumani inaingia kwenye list, Audi. Hii ilianzishwa mwaka 1909 na fundi makenika ajulikanaye kama August Horch. Tafsiri ya Kilatini, Audi ina maana ya “Sikia”, ambayo ni sawa na Kijerumani “Horch”. Jina Audi linawakilishwa na maduara manne kwenye Logo ya magari hayo ambayo yanaundwa na kampuni nne na ndio sababu za kuwekwa maduara manne kwenye Logo yake.
Audi inatajwa kuwa moja kati ya magari mazuri na ya kisasa, salama na yenye gharama pia; Na katika kuthibitisha hilo, Audi ilikuwa kampuni ya kwanza ya kuunda magari duniani kufanya majaribio ya magari yake kwenye ajali makusudi ili kujua yanaharibika kiasi gani.
7. Bugatti
Bugatti ni kampuni ya kuunda magari iliyoanzishwa na raia wa Italy aitwaye “Ettore Bugatti” na kwa mara ya kwanza ilianza kuunda magari nchini Ufaransa mwaka 1909. Aina hii ya magari ilipata umaarufu wa kuunda magari yenye speed zaidi duniani pia walihusika na kuunda ndege.
Wanarekodi pia ya kuwa kampuni kongwe zaidi ya uundaji magari; Bugatti wana sifa nyingine kuwa na magari yenye starehe zaidi na ya kipekee. Gharama sio jambo la kushangaa unapouliza bei za magari ya Bugatti na mwaka 1956 Bugatti waliingiza sokoni magari zaidi ya 8000, kitu ambacho kinaweka idadi ya kuwa wameshatengeneza zaidi ya magari 100,000 yaliyoko kwenye matumizi kote duniani.
6. Lamborghini
Lamborghini pia ni kampuni iliyoanziwa na fundi Muitaliano aitwaye “Ferruccio Lamborghini” mwaka 1963. Mwanzo kabisa kampuni hii ilikuwa ikiunda Matrekta kwaajili ya shughuli za kilimo. Baada ya Lamborghini kufariki mwaka 1993, kampuni hii haikuwa tena ya mtu binafsi, mwaka 1998, iliungana na kampuni nyingine mbili Audi pamoja na Volkswagen.
5. Ford
Ford Motor Company ni moja kati ya makampuni ya kuunda magari yanayoheshimika sana duniani ikiwa ni kampuni kongwe zaidi ya Kimarekani inayounda magari yenye sifa ya uimara. Kampuni hii ilianzishwa na Henry Ford mwaka 1903. Kitu cha kushangaza kuhusu Ford kwa kipindi cha miaka 6 haikuwahi kutengeneza magari yenye rangi nyeusi.
Hayo yalikuwa maamuzi ya mmiliki wake, Henry Ford aliyekuwa akifanya kazi kama Engieer kwenye kampuni ya Edison Illuminating Company akiwa kama Mhandisi Mkuu. Kama ilivyo historia za makampuni mengi ya uunndaji magari, Ford pia walikuwa wakiunda ndege; na kampuni yake iliitwa Ford Airplane Company, lakini haikufanikiwa kupata faida kitu kilichofanya ifungwe kabla haijasababisha hasara.
4. Ferrari
Ferrari pia ni kampuni ya Kiitaliano ambayo imejikita kwenye kuunda magari yanayotumiwa kwenye michezo ya mbio za magari. Kampuni hii ilianzishwa na fundi makenika aitwaye “Enzo Ferarri” mwaka 1939. Ferarri ilianzishwa na mvulana wa miaka 10 tu mwenye jina la Enzo, ambaye alikuwa mpenzi wa mbio za magari aliyekuwa na ndoto za kuja kumiliki kampuni yake na alitimiza ndoto yake.
Brand ya Ferrari inarekoi ya kuwa kampuni inayozaliwa magari ya michezo yenye gharama kubwa, speed, ya kisasa na imara zaidi ya muda wote duniani. Ile logo ya njano yenye picha ya Farasi kwenye magari ya Ferrari ilikuwa inatumiwa na kamanda wa kwanza kutoka jeshi la Italy wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia, Francesco Baracca.
Wakati huo Enzo Ferrari alimuomba Baracca aitumie logo hiyo ili kumtangaza kama mtu mwenye bahati; sasa miaka kadhaa baada ya kifo cha Kamanda wa jeshi Baracca logo hiyo imekuwa ni utambulisho rasmi wa magari ya Ferarri.
3. Porsche
Porsche pia ni kampuni iliyonunuliwa na kampuni ya Kijerumani ya Volkswagen Group.Ilianzishwa mwaka 1931 na fundi mitambo Ferdinand Porsche. Ikiwa moja kati ya kampuni maarufu za kuunda magari, Porsche pia haikuanzia kwenye kutengeneza magari, ilikuwa ikifanya kazi ya kushauri namna nzuri ya kuunda magari.
Miaka 10 baadaye, ikajikita kwenye kuunda magari yanayotumika kwenye michezo. Magari ya Porsche yameweka rekodi ya kushinda karibia mashindano zaidi ya 30,000 ya mbio za magari, kiwango ambacho hakuna kampuni au brand yoyote ilifikia rekodi hiyo mpaka sasa. Porsche wanajulikana kwa kuwa na magari ya kipekee duniani.
2. Bentley
Bentley Motor Limited, inafahamika zaidi kwa jina la Bentley, ni kampuni ya kuunda magari iliyoanzishwa na raia wawili ambao ni ndugu kutoka Uingereza H. M. Bentley na Walter Owen Bentley mwaka 1919, na baadaye ikanunuliwa na Volkswagen Group mwaka 1998.
Bentley wamejiwekea rekodi ya kuunda magari ya kisasa na mengi yamekuwa yakitumiwa na watu maarufu wakiwemo mastaa wa muziki, filamu, michezo, viongozi wa taasisi n.k.Bentley pia ni kati ya brands zinazoongoza kwa kutoa misaada kwenye maeneo mbalimbali duniani.
1. Volkswagen
Volkswagen, inajulikana kwa ufupisho wa jina lake kama ‘VW’, hii ni gari inayotengenezwa na kampuni kutoka Ujerumani ambayo ilianzishwa mwaka 1937 na chama cha wafanyakazi cha German Labour Front. kitu cha kushangaza kuhusu Volkswagen ni kwamba wazo la kuundwa kwake liliwekewa mkazo na mtawa wa mabavu, Adolf Hitler.
Tafsiri ya neno Volkswagen ni ‘Gari ya Watu’, na slogan yake ni ‘Das Auto’ ikiwa na maana ya ‘Gari’ kwa lugha ya Kijerumani, kinachobebwa kwenye maneno yote hayo ni kumaanisha kwamba gari yao ni mfano sahihi wa jinsi gari inavyotakiwa kuwa.
Inasemekana Volkswagen ndiyo kampuni ya kuunda magari ambayo ni kubwa kuliko zote kwasasa. Kingine ni kwamba VW wanashikilia rekodi ya kuwa kampuni inayounda magari ya kisasa zaidi duniani, pia wanaunda magari ya mizigo; sio tu kubeba mizigo magari yake makubwa yanauwezo wa kufanya mashindano ya mbio.