Matunda
Kisukari ni ugonjwa ulioingia
kwa kasi nchini. Ni hali inayotokea wakati sukari inapozidi ile
inayotakiwa katika damu kwa sababu ya upungufu au ukosefu wa Insulin.
Insulin ni kichocheo kinachotengenezwa kwenye kongosho na kwamba
hutumika kusaidia mwili kutumia sukari inayotokana na vyakula
tunavyokula.
Kuna aina kuu mbili za kisukari
Kwanza ni kisukari kinachotegemea
Insulin. Kazi ya Insulin ni kurekebisha hali ya sukari kwenye damu,
ikiwa ni nyingi inapunguzwa kurudi kwenye hali ya kawaida na ikiwa
chache huruhusu irejee kwenye hali ya kawaida pia. Kunapokuwa na
hitilafu kongosho likazalisha homoni hii kwa wingi, sukari hupungua
mwilini, au isipozalishwa, sukari huongezeka mwilini. Hospitalini, aina
hii ya sukari inatibiwa kwa kutumia sindano za Insulin na kurekebisha
ulaji wa vyakula.
Pili ni kisukari kisichotegemea Insulin.
Hospitalini hiki huthibitiwa kwa kutumia vidonge pamoja na kurekebisha
ulaji wa vyakula au kwa kurekebisha vyakula peke yake. Watu wengi walio
na aina ya kisukari kisichotegemea Insulin ni wanene kupita kiasi na
ikiwa watapunguza uzito kasi ya ugonjwa hupungua au kwisha kabisa.
Sukari inaweza kuwa juu au chini kupita kiasi cha kiwango kinachotakiwa.
Hali zote hizo mbili si nzuri kwa
binadamu kwa sababu mgonjwa anaweza kufa haraka. Sukari inaweza kuwa juu
bila dalili zozote zile kujitokeza mwilini mwa mgonjwa. Watu wanaojijua
kuwa na tatizo la kisukari wanashauriwa kupima damu au mkojo mara kwa
mara ili kufahamu kama sukari katika damu yao iko sawa au haiko sawa.
Dalili za mtu aliyepungukiwa sukari
mwilini ni pamoja na mapigo ya moyo kwenda haraka haraka, kutokwa jasho
kwa wingi, kujisikia kama mwenye homa, kuchoka kukojoa mara kwa mara na
kuumwa kichwa. Ni vizuri mtu akihisi dalili hizo ahakikishe anapima
sukari mwilini. Hadi sasa hakuna tiba ya kuponya ugonjwa wa kisukari.
Hata hivyo, wagonjwa wote wanaweza
kuishi vizuri na kufanya kazi zao zote ikiwa watafuata maelekezo na
masharti yanayotakiwa. Madhara ya kisukari ni kwamba mtu mwenye kisukari
anaweza kupatwa na tatizo la kupungua uwezo wa macho kuona, figo
kutofanya kazi zake ipasavyo na kupata vidonda vya miguuni visivyopona
kwa wanaume kuwa na upungufu wa nguvu za kiume.
Pia mtu mwenye tatizo la kisukari
mishipa yake ya fahamu ya miguuni na mikononi kutofanya kazi zake
vizuri, matatizo ya moyo na kupatwa na magonjwa mbalimbali ya ngozi.
Madhara hayo yanazuilika kwa kuzingatia kutozidi kwa sukari kwenye damu
ya mgonjwa.
Ushauri kuhusu chakula kama una
kisukari, vyakula vinavyofaa husaidia mwili kuwa na viwango vya sukari
na mafuta vinavyostahili kuwepo damuni, hupunguza unene kupita kiasi,
hutosheleza mahitaji ya mwili ya nishati, madini na vitamini ili
kuuwezesha mwili kuwa na uzito unaostahili na kufanya kazi ipasavyo.
Matunda na mboga
Kila mwenye tatizo la ugonjwa wa
kisukari anatakiwa kuepuka kula vyakula vilivyowekwa sukari kwa sababu
sukari huyeyushwa upesi sana tumboni na kusababisha sukari nyingi
kuingia kwenye damu katika muda mfupi. Vyakula kama sukari, glucose,
asali, jamu, keki, pipi, ice cream, chocolate na soda zote zilizo tamu
haviruhusiwi kwa mtu mweye tatizo la kisukari.
Chai, kahawa, maziwa na uji vinaruhusiwa
kutumiwa iwapo vitakuwa havijaongezwa sukari. Madafu na club soda
vinaruhusiwa kwa sababu havina sukari inayoweza kuyeyuka haraka na
kukimbilia kwenye damu.
Mgonjwa wa sukari anaweza kuongeza utamu
kwenye mchanganyiko anaoutaka kwa kutumia vidonge maalum ambavyo
hupatikana kwenye maduka ya madawa.
Njaa nayo huchangia kumfanya mgonjwa wa
kisukari kujisikia vibaya huenda kwa vile sukari inaweza kupungua kupita
kiasi mwilini.Mgonjwa wa kisukari anatakiwa kutokaa na njaa, kula mara
kwa mara na pia kula mara tatu au zaidi kwa siku na ikiwezekana
anatakiwa kutafuna vitu vidogo vidogo katikati ya milo mikubwa.
Inashauriwa kuwa mgonjwa asipendelee
kula milo mikubwa mchana au jioni. Mgonjwa huyo hatakiwa kuacha kula
vyakula vyenye wanga kama vile ugali, viazi na wali. Anachotakiwa
kufanya ni kuzingatia kiasi cha chakula cha wanga anachokula kwa mlo na
pia anatakiwa kutumia zaidi nafaka zisizokobolewa kwa mfano dona kwa
sababu huweza kumpatia mgonjwa vitamini na madini. Hakuna sababu ya
mgonjwa kupikiwa chakula chake maalum kwa sababu anaweza kula chakula
chochote kilichopikwa na familia isipokuwa vile vilivyowekwa sukari.
Ice Cream
Mgonjwa anatakiwa kula matunda kwa wingi
na kwamba anaweza kula matunda aina zote kwa siku. Anatakiwa pia kula
mboga za majani kwa wingi au kachumbari kila siku. Mgonjwa wa kisukari
anatakiwa kupunguza kiasi cha mafuta anachokula na pia kuepuka kula
mafuta yenye asili ya nyama. Anatakiwa kutumia zaidi vyakula
vilivyochomwa, kuokwa au kubanikwa kuliko vile vilivyokaangwa na kula
samaki, maharage au kuku aliyetolewa ngozi.
Mgonjwa wa kisukari anatakiwa kuepuka kunywa pombe kwa wingi kwa sababu huweza kuathiri afya.
Vyakula vinavyoweza kumwongezea mgonjwa
madhara ni sukari yenyewe, nyama yenye mafuta, figo au maini husababisha
sukari kupanda kwa kiwango cha aina ya mafuta mabaya yanayosababisha
damu kuganda kwenye moyo na mishipa ya damu na kuleta magonjwa ya moyo.
Vyakula vya kuliwa bila masharti ni
mboga za majani, nyanya, matango, bamia, karoti, vitunguu, pilipili
hoho, pilipili, viungo vyote vya vyakula bila kuweka chumvi nyingi, maji
ya kunywa, chai na kahawa.Ikiwa mgonjwa wa kisukari anaumwa na hawezi
kula vyakula vya kawaida anatakiwa kunywa uji, maziwa na maji ya
matunda.