SHAHIDI wa tatu, Konstebo wa Polisi (PC), Juliana Moses (31), ameieleza mahakama kuwa aliwapekua mshtakiwa Mwanaidi Mfundo, maarufu kama Mama Leila, na Sara Munuo katika vyumba vyao vya kulala na kupata pakiti nne za unga uzaniwao kuwa dawa za kulevya, fedha na hati tatu tofauti za kusafiri.
Aidha, PC Moses alidai kuwa kabla ya upekuzi huo alifika nyumbani kwa Mama Leila Mei 31, 2011 kati ya saa mbili na saa tatu usiku akiwa na polisi wenzake pamoja na mkuu wake, Kapufi, na kufanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi washtakiwa wanane.
PC Moses alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kuingiza nchini dawa za kulevya zenye thamani ya sh. milioni 225, mbele ya Jaji Isaya Arufani.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo na Wakili wa Serikali, Paulina Mwangamila.
Akiongozwa na Kakolaki, shahidi alidai kuwa siku ya tukio aliambatana na askari wenzake wakiongozwa na kiongozi wao Kapufi kwenda kwenye kazi maalum.
"Afande alisema tunakwenda Mbezi Beach kwenye tukio, tulipofika tukaacha magari tukatembea hadi kwenye nyumba ya mshtakiwa wa kwanza," alisema PC Moses na kueleza zaidi:
"Tulifanikiwa kuizunguka nyumba kuiweka kwenye usalama, afande Kapufi aligonga mlango akajitambulisha ni askari lakini tulisubiri muda wa nusu saa bila kufunguliwa mlango.
"Tulipochungulia ndani tuliona watu wakizunguka huku na kule ndipo afande akagonga na kuwaarifu wasipofungua atavunja mlango.
"Mlango ulifunguliwa na mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Mwanaidi ama Mama Leila; aliwekwa chini ya ulinzi na wote waliokuwa ndani ya nyumba ile."
Akifafanua zaidi, alidai kuwa waliamrisha wote walioko ndani watoke nje, wakatoka watu wanane akiwamo Mama Leila.
Ifuatayo ni sehemu ya mwongozo kati ya wakili wa Jamhuri na shahidi:
Wakili: Baada ya kuwaweka chini ya ulinzi nini kilifuata?
Shahidi: Afande Kapufi alimtaka Mama Leila kumwelekeza makazi ya mjumbe wa eneo hilo kwa ajili ya kushuhudia upekuzi.
Hata hivyo, Mama Leila aligoma kutoa maelekezo kwa madai kuwa miongoni mwa wale walioko chini ya ulinzi atakuwa shuhuda wake.
Wakili: Kwanini aligoma?
Shahidi: Mama Leila alisema anaepuka aibu kwa majirani, lakini afande alikataa utetezi wake ndipo akakubali kutoa maelekezo.
Afande aliwaagiza askari wawili kati yetu, kwenda kwa mjumbe lakini walirejea wakiwa na wajumbe wawili wa jirani, baada wa yule anayehusika na eneo lile kudaiwa kuwa ameingia kazini usiku.
Wakili: Je, nini kilitokea?
Shahidi: Afande alijitambulisha kwao na kuwaeleza nia na madhumuni ya kuwaita ni kutaka wasimamie upekuzi wa nyumba ile.
Wakili: Mlipekua?
Shahidi: Ndiyo, afande alimtaka Mama Leila kutuelekeza chumba chake cha kulala, mimi, wajumbe na mwenyewe bosi, alikubali kutuongoza nikaanza kumpekua.
Wakili: Ulifanikiwa kupata chochote?
Shahidi: Ndiyo, kitandani kwake Mama Leila, kati ya godoro na chaga nilikuta pakiti mbili zilizokuwa zimeandikwa 'Coffee Care Orginal' zilizokuwa na unga uzaniwao dawa za kulevya, hati moja ya kusafiria, fedha za Kitanzania, Kenya na dola za Kimarekani.
Pia, nilimpekua Munuo chumbani kwake; nilifanikiwa kupata pakiti moja kwenye kabati la nguo, nyingine ya pili chooni ndani ya sinki la kusukumia maji zenye unga uzaniwao kuwa dawa za kulevya, hati mbili za kusafiria, ikiwamo ya Kenya.
Kesi hiyo inaendelea na ushahidi wa upande wa Jamhuri leo.
Mapema mahakamani hapo, shahidi wa kwanza Mkemia Mkuu Daraja la Kwanza, Bertha Mamuya alidai kuwa alipofanyia uchunguzi pakiti mbili zilizokuwa na maandishi ya 'Coffee Care Orginal' na ile pakiti iliyotolewa chooni zilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin na ile pakiti moja iliyotolewa kwenye kabati la mshtakiwa Munuo ilikuwa na dawa za kulevya aina ya cocaine.
Mbali na Mama Leila na Munuo, washtakiwa wengine ni, raia wa Kenya Anthony Karanja na Ben Macharia, na Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Mzome na John William.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa mwaka 2011, wanadaiwa kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya sh. milioni 225.