Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema licha ya uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia saba kwa zaidi ya muongo mmoja, bado hali ya uchumi ni mbaya Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa takwimu jijini Dar es Salaam jana, Dk Mpango alisema ili kupambana na umaskini, Serikali imejikita kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira.
Alitaja takwimu za Benki ya Dunia (WB) za mwaka 2013 akisema asilimia 10.7 ya watu wote duniani ambao ni bilioni 7.1 walikuwa wakiishi chini ya Dola 1.90 za Marekani kwa siku ikilinganishwa na asilimia 12.4 mwaka 2012. “Mbali na takwimu hizo kuonyesha umaskini kushuka kwa kasi ndogo, mafanikio hayo hayaonekani waziwazi kwa baadhi ya nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania,” alisema.
Alisema hali hiyo inatokana na ukuaji wa uchumi kutokana na sekta zinazoajiri watu wachache na nyingi zikijikita mijini na kuwapo kwa kasi ya ongezeko la watu.