NCHINI Marekani kila baada ya dakika 10 mtu mmoja huwekwa kwenye foleni ya watu wanaosubiri kuwekewa moyo mpya ili kuweza kuendelea kuishi. Hali hii hotokea baada ya moyo wa mgonjwa kuonekana hauwezi kufanyiwa matibabu na hivyo njia pekee ya kuokoa maisha yake ni kupata moyo mpya ambao huwekewa kwa njia ya upasuaji (transplant).
Shirika la Umoja wa Kuchangia Viungo, linasema kuwa takribani watu 22 hufariki dunia kila siku nchini Marekani wakiwa katika foleni ya kusubiri mtu wa kujitolea moyo kwa ajili ya kuokoa maisha yao. Hata hivyo, wagonjwa wa aina hii sasa wanaweza kufurahia baada ya ugunduzi wa moyo wa bandia ambao inawezekana wakautumia kwa maisha yao yote (Total Artificial Heart)TAH).
Mtu anayechangia moyo (donor) anaweza kuwa ni mtu ambaye tayari ubongo wake umekufa lakini mwili bado una uhai na hivyo moyo wake kuwa mzima. Mgonjwa wa aina hii hawezi kupona. Mgonjwa yeyote ambaye ana hali mbaya lakini ugonjwa wake hauhusiani na moyo na ambaye hawezi kupona pia anaweza kujitolea moyo. Mtu aliyefariki pia anaweza kutolewa moyo na kusaidia wenye uhitaji lakini mara nyingi hii huwa ni kwa ridhaa yake kabla hajafariki.
Ukiwa umegunduliwa kwa mara ya kwanza takribani miaka 60 iliyopita, moyo wa bandia wa wakati huo uliwawezesha wagonjwa waliokuwa wakisubiri kupata mtu atakayejitolea kupatikana na uliweza kumsaidia mgonjwa kwa muda tu. Ugunduzi huu mpya, unaweza kutoa suluhisho la kudumu kwa kuwa moyo huo unalenga kumwezesha mgonjwa kuishi maisha yake yote.
Historia inaonyesha kuwa, kipindi kirefu ambacho mgonjwa ameweza kuishi kwa msaada wa teknalojia ya moyo wa bandia uliojulikana kitaalamu SynCardia temporary TAH ni miaka minne.
Katika kile ambacho kinaelezwa kama hatua nzuri ya ugunduzi, Kampuni inayohusika na matatizo ya moyo ya nchini Marekani inayojulikana kama SynCardia Systems Inc inaendesha utafiti na kufanya uchambuzi wa kina kuona kama TAH inaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa wagonjwa wanaohitaji kubadilishiwa moyo na kushindwa kuupata kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa mahitaji.
“Mwishoni mwa miaka ya 1960 wakati wagonjwa walipoanza kuwekewa mioyo mipya kutoka kwa binadamu wengine, upatikanaji wa kiungo hicho muhimu kwa maisha ya binadamu ulikuwa mkubwa. Upatikanaji wake ulikuwa mkubwa kuliko mahitaji lakini kwa sasa mahitaji yameongezeka zaidi na upatikanaji umepungua,” anasema Danald Isaacs ambaye ni Makamu wa Rais wa SynCardia, akiliambia Shirika la Habari la Fox.com.
Idara ya Afya na Huduma za Binadamu ya Marekani inakadiria kuwa watu 4,000 husubiria kupata moyo mpya ili waweze kuendelea kuishi kila siku wakati mioyo 2,300 ikiwa inatolewa.
Ugonjwa wa moyo ni chanzo namba moja cha vifo nchini Marekani ukigharimu maisha ya watu 611,000 mwaka 2015, hii ni kwa mujibu wa Kitua cha Kupambana na Kuzuia Magonjwa cha nchi hiyo (CDC)
Wakati wa kumwekea mgonjwa moyo wa bandia au TAH, daktari huondoa kwa njia ya upasuaji ventrikali ya kulia pamoja na valvu nne kama ambavyo hufanyika wakati mgonjwa akiwekewa moyo ambao hutolewa na binadamu mwingine ambapo huwekwa wa bandia badala yake.
“Asilimia 96 ya mfumo wa kuweka moyo bandia ni ule wa SynCardia Temporary TAH ambao hutoa suluhisho la muda tu,” anasema Isaacs. Takwimu za SynCardia zinaonyesha kuwa wagonjwa 1,123 wamewekewa mfumo huo ambao ni modeli 70cc.
John Beckingham, mwenye umri wa miaka 58 ambaye ni mhandisi mstaafu anayeishi katika eneo la Rochester jijini New York alifanyiwa upasuaji uliofanikisha kuwekewa moyo mpya katika hospitali ya Cleverland, Oktoba mwaka 2015 baada ya kukaa miezi sita kwenye foleni ya kusubiria. Wakati akisubiria alikuwa akitumia mashine maalumu ambayo ilikuwa ikitumia betri na ambayo ufanisi wake haukuwa sawa na teknalojia hii mpya.