Tetemeko la ardhi ya ukubwa wa 5.7 kwenye vipimo vya Richter limekumba maeneo ya Ziwa Tanganyika mapema Ijumaa.
Tetemeko hilo lilitikisa maeneo ya kaskazini mwa Zambia na mitetemeko hiyo ikasikika maeneo ya kusini magharibi mwa Tanzania.
Kitovu cha tetemeko hilo, kwa mujibu wa Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani, kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi umbali wa kilomita 45 kutoka mji wa Kaputa nchini Zambia.
Mji huo unapatikana katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Tetemeko hilo lilitokea mwendo wa saa tisa na dakika thelathini na mbili usiku (0032 GMT).
Tetemeko la ardhi la ukubwa kama huo huchukuliwa kuwa la kadiri lakini wataalamu wanasema kutokana na hali kwamba kitovu chake chakikuwa chini sana ndani ya ardhi, huenda hilo lilisababisha mitikisiko kuwa mikubwa.
Desemba mwaka 2005, tetemeko kubwa la ardhi lilitokea eneo la Ziwa Tanganyika.
Tetemeko hilo la nguvu ya 6.8 lilitikisa majumba katika miji maeneo ya Afrika mashariki na kati.
Sehemu kubwa ya maeneo ya Afrika Mashariki huwa katika Bonde la Ufa, bonde kubwa lililoundwa kutokana na kuhama kwa maeneo makubwa ya ardhi na milipuko ya volkano.
Hilo huyafanya kuwa hatarini ya kukumbwa na mitetemeko ya ardhi.
Septemba mwaka 2016, tetemeko jingine la ardhi lililotokea eneo la Bukoba, mkoani Kagera kaskazini mwa Tanzania.
Watu 16 walifariki na wengine 250 kujeruhiwa kutokana na tetemeko hilo. Mamia wengine walibaki bila makao.
Tetemeko hilo la ukubwa wa 5.7 kwenye vipimo vya Richter, lilitajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kukumba taifa hilo la Afrika Mashariki katika kipindi cha zaidi ya mwongo mmoja.