Baadhi ya simulizi za watu humhusisha ndege aina ya Bundi na mikosi, hali hiyo inaweza pengine kuwa tafsiriwa ya matukio ya kuanguka kwa vifusi kwenye machimbo ya madini nchini.
Janua 25, Wachimbaji wadogo 15 katika Mgodi wa Dhahabu wa RZ uliopo Kata ya Nyarugusu mkoani Geita walifukiwa na kifusi, lakini walifanikiwa kuokolewa baada ya siku tano.
Februari 13, wachimbaji sita walifukiwa na kifusi katika machimbo ya dhahabu Buhemba mkoani Mara, miili ya watu wawili iliopolewa huku minne hadi sasa haijaonekana.
Tukio la hivi karibuni, watu wanne wamefariki dunia na wengine saba kunusurika baada ya kifusi kuwafukia kwenye mgodi wa dhahabu machimbo ya Kijiji cha Itumbi, Wilaya ya Chunya mkoani Songwe.
Waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Simon Majaliwa (26) mkazi wa Itumbi, Mazoea Mahona (25) kutoka mkoani Tabora, Ben Bahati (23) wa Mapogoro wilayani hapa na James Alinanuswe (26) wa Ushirika wilayani Rungwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari aliwataja waliojeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kuwa ni Mark Fredrick (22) mkazi wa Itumbi, Isack James (30) wa Mwanjelwa, Hamis Mourice (25) wa Mapogoro na Andrea Paul (26) wa Itumbi.
Kidavashari alisema wengine watatu ambao walijihisi kutokuwa na majeraha walikimbia na kwamba, tukio hilo lilitokea Februari 18 jioni na jitihada za uokoaji zilianza na kukamilishwa siku iliyofuata asubuhi.