MKUTANO wa Sita wa Bunge la 11 uliomalizika Ijumaa iliyopita mjini hapa, umeandika historia nyingine kutokana na kuwepo kwa mambo makuu matano yaliyolipa Bunge hilo sura tofauti na mikutano mingine iliyopita.
Kwa pamoja wabunge wote bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa walisimamia walichokiamini hivyo kukipa chombo hicho hadhi yake.
Mambo hayo ni pamoja na kupinga wakuu wa mikoa na wilaya kuingilia haki na madaraka ya Bunge, wabunge kukamatwa bila utaratibu, kasoro katika kutaja watu wanaotakiwa kuhojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya, kuhoji utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 na kusuasua kwa utekelezaji wa sera ya Tanzania kuhusu viwanda.
Tofauti na mikutano iliyopita, mkutano huo ulishuhudia wabunge wakiungana katika hoja hizo bila kujali itikadi zao, jambo ambalo liliwaweka katika wakati mgumu baadhi ya mawaziri huku Spika Job Ndugai akihitimisha kwa kuonya wateule wa Rais wanaojisahau kwa kutoa lugha zisizoeleweka.
Madaraka ya Bunge
Kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuita mkutano wa waandishi wa habari na kuwataja watu kadhaa akiwataka kufika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, ndicho kilichoibua hoja ya kuingiliwa na kupuuzwa kwa madaraka ya Bunge.
Mjadala kuhusu suala hilo uliibuliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) kupitia kanuni ya 52.
Katika hoja yake, Waitara alisema Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti walitoa matamshi yanayoingilia haki na madaraka ya Bunge.
Waitara alisema Makonda wakati akizungumza na wanahabari, alisema wabunge huwa wanakwenda bungeni kusinzia, kauli ambayo inakiuka Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Kuhusu Mnyeti, alisema mkanda wa video yake umesambaa katika mtandao wa facebook ukimnukuu akisema; “huu ni upuuzi mtupu, wabunge hawa hawajielewi nawashauri mfanye kazi zenu.”
Hoja ya Waitara ambayo siku moja nyuma iliibuliwa na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM) na Bunge kuazimia Makonda kuandika maelezo ya kujieleza kwa kauli yake hiyo ambapo iliungwa mkono na wabunge wote na kutaka hatua zichukuliwe ili kurejesha hadhi ya mhimili huo.
Baada ya Waitara kutoa maelezo yake, wabunge mbalimbali walichangia na kubainisha kuwa Serikali haiwezi kujengwa na viongozi wenye kiburi.
“Unapotaka kulitoa pepo mheshimiwa mwenyekiti halibembelezwi. Unataka kuyapunga majini huwezi kubembeleza. Lazima ukazane kulipunga jini litoke. Hatuwezi kutoa pepo kwa lugha nyepesi nyepesi (akipunguza sauti) pepo toka, haiwezekani. Kama ni pepo tulikemee litoke,” alisema John Kidutu, Mbunge wa Ulyankulu (CCM).
Hoja hiyo ilihitimishwa kwa Bunge kupitisha maazimio manne bila kusikia sauti ya “siyooo” kutoka miongoni mwa wabunge, likiwemo la kuwaita wateule hao wawili wa Rais kuhojiwa na mhimili huo kwa matamshi yao.
Wabunge kukamatwa
Hoja ya wabunge kukamatwa bila Bunge kuwa na taarifa lilikuwa ni moja ya maazimio hayo manne yaliyopitishwa kwenye mkutano huo, huku Spika wa Bunge, Ndugai wakati akiahirisha Bunge aliagiza mtu anayemtaka mbunge ni lazima atoe taarifa kwake.
Ndugai alionya kuwa,“wakati mwingine akikosekana mbunge mmoja inawezekana mambo kwenye kamati yasitekelezwe. Kwa hiyo kama kuna ofisa yeyote anamhitaji mbunge, lazima aniambie. Hatuwezi kwenda hivyo. Kwa hakika kwenda hivyo kibabebabe kutaivuruga nchi.”
Kutajwa majina
Sakata la kutangaza hadharani majina ya watu wanaotakiwa kuhojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya ililiwaamsha wabunge na kutoa kauli zilizoonesha kutokubaliana na utaratibu unaotumika katika vita dhidi ya dawa hizo haramu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu wakati akihitimisha michango ya wabunge kuhusu taarifa ya kamati hiyo alisema:
“Upelelezi wa kesi za jinai hauwezi kufanywa kwa kutaja majina ya watu hadharani. Kufanya hivyo ni kupoteza ushahidi mahakamani.”
Utekelezaji bajeti
Katika mkutano huo kamati mbalimbali za Bunge ziliwasilisha taarifa za kuanzia Januari 2016 hadi Januari mwaka huu, huku kukiwa na upungufu mkubwa katika utekelezaji wa bajeti za maendeleo katika wizara mbalimbali.
Katika uchambuzi uliofanywa na gazeti hili hakuna wizara hata moja iliyopata asilimia 45 ya bajeti ya fedha za maendeleo, jambo ambalo wabunge walihoji na kueleza wasiwasi wao kuhusu utekelezaji huo.
Mathalan, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji hadi kufikia Januari mwaka huu imepatiwa sh. bilioni 7.6 ya fedha za maendeleo sawa na asilimia 18.6.
Licha ya fedha hizo kutotolewa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alilieleza JAMBO LEO kuwa Serikali inatekeleza bajeti yake kulingana na inavyokusanya na kusisitiza kuwa miradi mingine ya maendeleo ni endelevu.
“Utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa awamu. Hivyo ndivyo ilivyo, mfano ujenzi wa darasa unakuwaje? ni suala la awamu tu,” alisema Dk. Mpango.
Tanzania ya Viwanda
Suala la Tanzania kuwa nchi ya viwanda nalo lilitikisa Bunge huku wabunge wakionesha wasiwasi hao kama sera hiyo itatekelezeka.
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alisema Serikali haiwezi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama haijajua sababu zilizoua viwanda vilivyokuwapo.
Alisema badala ya Serikali kusisitiza uanzishwaji wa viwanda vipya, ingeimarisha viwanda vilivyopo ili vizalishe kwa mafanikio zaidi kwa sababu baadhi havina malighafi za kutosha.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage naye alijikuta katika wakati mgumu baada ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kusema haina taarifa yoyote ya kuanzishwa kwa viwanda 1,169 nchini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Dalaly Kafumu alisema, “Viwanda ambavyo vimesemwa na Ulega ni 67, Waziri anasema ana viwanda 1,169. Mimi nataka niseme hili, kamati yangu haina taarifa kabisa,”alisema Dk Kafumu.
“Tafsiri yetu kama kamati ni kuwa waziri hushirikiani na sisi vizuri kwa sababu tungekuwa tuna habari hata kufunguliwa kwa kiwanda cha Mkuranga. Tungejua angeweza kwenda mwenyekiti wa kamati au hata mjumbe mmoja tu. Habari tungekuwa nazo.”