CCM Yamweka Kiporo Yusuf Manji

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Temeke, kimesema hakitamjadili Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Yusuph Manji, hadi kesi yake kuhusu madai ya kutumia dawa za kulevya itakapomalizika mahakamani.

Msimamo huo umetolewa baada ya kuwapo  taarifa kwamba chama hicho kimepanga kumjadili Manji kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Taarifa hizo zilieleza kuwa diwani huyo atajadiliwa vikaoni ili afukuzwe uanachama kwa kuwa chama hicho hakitaki wanachama wenye tuhuma na wanaovunja amri za nchi.

“Kikao cha kamati ya utendaji ya chama kitaitishwa mapema mwezi huu kutekeleza maazimio ya vikao vilivyokwisha kufanyika kuanzia tawi hadi kata ambavyo vilikuwa na agenda ya kumjadili Manji kuhusu tuhuma zake,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Jana, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Yahaya Sikunjema, alisema hawawezi kuingilia suala ambalo bado liko kwenye vyombo vya sheria.

“Wakati utakapofika na ikaonekana ipo sababu baada ya vyombo husika vya sheria kama mahakama kumtia hatiani.

“Kama chama tutakaa tuangalie katiba yetu inatuelekeza vipi na hapo ndipo tutachukua hatua,” alisema Sikunjema.

Wiki iliyopita Manji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akidaiwa kutumia dawa za kulevya.

Manji alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mumjadili Manji wakati nyie wenyewe maadili ZERO?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad