Muda mchache baada ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kutangaza majina ya baadhi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika katika mtandao wa biashara ya Madawa ya kulevya akiwemo kiongozi ya juu wa CHADEMA na kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, Uongozi wa CHADEMA umefunguka na kueleza namna ambavyo hawakupendezwa jinsi jina la kiongozi wao wa juu lilivyotajwa bila kufuata utaratibu.
Wakizungumza na waandishi wa habari Jumatano hii, CHADEMA wamedai wao hawapingi kutajwa kwa mkuu wao ila wanapiga utaratibu iliyotumika kutaja jina la kuingozi huyo wa juu wa chama hicho.
“Kimsingi katika majina mengi yaliyotajwa kuna jina la Mwenyekiti wa chama Mbowe, swala la utetezi wake au maelezo hilo ni swala binafsi sababu kilichotajwa ni jinai lakini kimsingi tunachukua nafasi hii kulaani,” alisema mmoja kati ya viongizi hao.
“Tunalaani jinsi tusivyoweza kuendesha utawala wa sheria kwenye nchi yetu na jinsi tusivyofata kanuni zilizowekwa dhidi ya sheria, Mh. Mbowe ni kiongozi wa kitaifa, ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, ni Mbunge wa Hai…. kwahiyo kuna taratibu za kufata unapokua na kusudio la kumuita,”
Aliongeza, “Kitendo cha kwenda kuongea kwenye mkutano na Waandishi wa habari na kutaja viongozi wakuu wa kitaifa ambao wana tuhuma tu ambazo hazijathibitishwa, ni kukosa ustaarabu wa kiuongozi, tusingependa kuona viongozi wengine waandamizi kutendewa kama alivyotendewa kiongozi wa chama chetu,”
Pia katika list hiyo mpya ya Makonda ametajwa aliyekuwa Mbunge wa CCM, Iddi Azzan, mchungaji Gwajima pamoja na watu wengine.