Shahidi wa nne katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njwete, ameieleza Mahakama kuwa mtu aliyehusika kumtoa macho Said Mrisho alikuwa ni mzoefu wa vitendo hivyo na siyo wa kawaida.
Shahidi huyo, Dk Christine Mataka (52) ambaye ni daktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alitoa maelezo hayo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala alipotoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa Njwete (34) katika kesi iliyopata umaarufu wa ‘kesi ya Scorpion’ kutokana na maelezo kwamba aliyefanya uhalifu huo ni Scorpion.
Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga, Dk Mataka kutoka kitengo cha macho alidai ilikuwa mara yake ya kwanza kuona mgonjwa aliyepelekwa Muhimbili akiwa hana vipande vya gololi za macho yote mawili.
Dk Mataka alidai mlalamikaji Said aling’olewa macho kwa kutumia kitu kikali kilichojikunja mbele ambacho kinaweza kutoa mboni ya jicho nzima bila kubaki kitu chochote.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule alidai kwa kawaida wagonjwa wanaopasuka jicho huwa wanakuwa na mabaki au vipande vya gololi ya macho.