Duh..Eti Serikali Itatumia Bilioni 105 kwa Ajili ya Kutunzia Nyayo za Binadamu wa Kale..!!!


WIZARA Maliasili na Utalii inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufukua nyayo za Laetoli zilizopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro zilizogunduliwa na mtafiti Dk Mary Leakey mwaka 1978.

Jitihada hizo za wizara zinafanywa kutokana na agizo la Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwaka 2007, alipoitaka wizara hiyo kufukua nyayo hizo na kuzihifadhi kisasa kwa matumizi ya elimu na utalii kwa Watanzania na wageni.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mchafu Chakoma (CCM) aliyetaka kujua serikali inafanya mkakati gani kuajiri wataalamu wa kufukua nyayo hizo.

Makani alisema, mradi huo una gharama kubwa unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 50 (sawa na Sh bilioni 105), ambazo zitatumika kwa ajili ya kusomesha wataalamu na kuandaa michoro ya ujenzi wa makumbusho.

Lakini pia fedha hizo zitatumika katika kufufua na kuhifadhi nyayo hizo, kusimamia ujenzi na kuweka mifumo ya uhifadhi wa kisasa wa nyayo hizo.

Alisema fedha hizo ni nyingi, ukilinganisha na mapato na majukumu ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambayo inatakiwa kugharamia, hivyo wizara inaendelea kutafuta fedha ili kugharamia utekelezaji wa mradi huo.

Makani alisema hakuna hali ya kusuasua katika kutekeleza mradi huo kwani baadhi ya kazi tayari zimekwisha kamilika na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kazi zilizokamilika ni pamoja na kuundwa kwa idara ya urithi wa utamaduni, kukamilika kwa michoro ya awali ya jengo la mapokezi, jengo la utafiti na jengo la elimu kwa umma.

Pia imewasilishwa tathmini ya athari kwa mazingira kwa mamlaka husika ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa uchambuzi wa kina ili kutoa idhini na kutoa mafunzo ya shahada ya uzamivu kwa watumishi wawili.

Kazi ambazo zinaendelea kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha taratibu za ajira kwa baadhi ya watalaamu wanaopatikana nchini na kukusanya takwimu sahihi kuhusu mazingira rafiki ya nyayo hizo na kazi inafanywa na watalaamu kutoka nje ya nchi inatarajiwa kukamilika Februari mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad