SERIKALI imeshauriwa kuanzisha mtaala wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kuwafundisha na kuwaandaa wanafunzi na namna ya kukabiliana na kuepukana na vitendo hivyo.
Akizungumza katika mdahalo wa kujadili vitendo vya ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria(WLAC), Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Fortunata Mtobi alisema kuingiza unyanyasaji wa kijinsia katika mitaala ya elimu kuanzia kwa watoto wa shule za msingi kutasaidia kujenga jamii yenye usawa na upendo.
Mtobi alisema kwa namna moja ama nyingine ukatili wa kijinsia umekuwa kama tatizo mtambuka kwa sababu unatoka na kurithishana.
“Kama mtoto anazaliwa, anakua anashuhudia vitendo vya ukatili wa kijinsia, baba anampiga mkewe au mtoto wa kike anafanyishwa kazi kuliko mtoto wa kiume, unafikiri akiwa mkubwa na yeye atafanya nini kama si kufuata yale aliyojifunza kutoka kwa waliomtangulia?” Alihoji Mtobi.
“Na ndio maana tunasema kama hakutafanyika jitihada za dhati kutokomeza hili, ikiwamo kuanza kuweka mfumo mzuri, kwa mfano mtaala wa kufundisha watoto kuanzia katika umri mdogo," alisema Mtobi na kufafanua, "itakuwa ni kazi kubwa kulitokomeza.”
Mratibu wa Kampeni ya Kupambana na Vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (Tunaweza) kutoka WLAC, Abia Richard alisema kwa kutumia pendekezo la Idara ya Ustawi wa Jamii, wasichana ambao ndio waathirika wakubwa na tatizo hilo watakuwa wamesaidiwa kuondolewa katika janga.
Alisema kuanzisha mtaala huo katika shule na vyuo, pia utasaidia wanafunzi na jamii kwa ujumla kuwa wawazi katika kutoa taarifa za vitendo hivyo.
“Pamoja na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali kupambana na suala hilo, ikiwamo kuielimisha jamii namna ya kupambana na tatizo hilo, lakini bado vinaendelea japo kuwa vimepungua tofauti na ilivyo kuwa hapo awali," alisema Richard.
"Tatizo ni kwa sababu wengine wanafundishwa kwamba vitendo hivyo ni vibaya ukubwani wakati katika maisha yao yote katika jamii zao wamekua wakishuhudia vitendo hivyo na ndio maana hata kuacha kwake ni hatua.
“Lakini tunaamini kwamba kama utakuwa ni utaratibu kuwaeleza watoto katika umri mdogo, itazoeleka na jamii itabadilika zaidi.
"Hakutakuwa tena na kusema hiki ni cha mwanamke au hiki ni cha mwanamke, wasichana na wavulana ama wanaume na wanawake wote watakuwa sawa.”
Serikali imetunga sera, sheria, miongozo na kuandaa mikakati mbalimbali katika jitihada za kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji.
Mikakati hiyo ni pamoja na Sera ya Wanawake na Maendeleo ya Jinsia (2000), Mkakati wa Maendeleo ya Jinsia (2005) na Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008).
Mingine ni Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (1998) na Sheria ya Mtoto (2009), vyote vikiwa na lengo la kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.