Dar es Salaam. Daktari bingwa mwandamizi wa Tiba na Afya ya Akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Frank Masao amesema mtumiaji aliyeacha ghafla matumizi ya dawa za kulevya hupata tatizo la arosto linalowasumbua sana.
Alisema mtumiaji anapokosa kilevi, arosto huwa kali zaidi siku tatu za kwanza, hupungua kati ya wiki moja hadi mbili na ili hamu ya matumizi ya dawa za kulevya imalizike kabisa huweza kuchukua hadi miaka miwili.
Hata hivyo, ameshauri kuwa watumiaji wanaoshikiliwa polisi wanapaswa kupewa matibabu kwa sababu dawa za kulevya zina madhara mwilini japo hawafi isipokuwa kuteseka.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu jana, Dk Masao alisema arosto ni kitendo cha mtumiaji wa kilevi kutamani au kuwa na kiu zaidi ya kukitumia kilevi hicho wakati anapokosa.
Dk Masao alisema arosto ya kila dawa hutofautiana na kwamba mtumiaji wa heroine anapokosa kilevi hicho, huanza kupiga miayo, kutoa machozi, kamasi, maumivu makali ya viungo, tumbo na kuharisha.
“Pia, huwa anakosa hamu ya kula, hapati usingizi, hofu isiyo na ulazima, hatulii sehemu moja, anakosa amani na huwa na hamu ya kilevi hicho kupindukia,” alisema.
Dk Masao alisema kawaida katika kichwa cha binadamu kuna sehemu inayoitwa ‘Mesolimbiq System’ au ‘Reward System’ ambayo ndiyo huwa inasababisha mtu kuendelea au kuiacha tabia fulani.
Alidai kuwa sehemu hiyo huwa inatoa kemikali inayoitwa Dopamine, hivyo ikiwa utatumia dawa za kulevya zozote zile huwa zinasababisha kemikali hiyo kutoka na kumfanya mtumiaji ajisikie raha zaidi.
“Kile kitendo cha kujisikia raha maana yake ni kwamba Dopamine imeachiliwa na isipoachiliwa utajisikia kinyume chake. Pia, huwa zinaacha kumbukumbu kwenye ubongo na baada ya muda raha hiyo ikiisha, mtu anatamani kuipata tena, hivyo ni lazima Dopamine itoke tena,” alisema.
“Ndiyo maana mtu anayetumia ulevu baada ya muda fulani anakuwa hana ujanja ni lazima atumie tena kilevi kwa sababu ‘Dopamine’ zinakuwa wazi. Ile hamu kupindukia ndiyo ambayo tunaita ‘arosto’ na hapo hulazimika kufanya kila kinachowezekana kupata kilevi,” alisema.
Aliongeza watumiaji wa dawa za kulevya wanapokuwa na arosto, hujikuta wakifanya vitendo vya uhalifu ilimradi wapate fedha za kununua dawa za kulevya kumaliza hamu waliyonayo.
“Ile hamu ya kuvuta kwenye ubongo wake huwa inakaa hadi miaka miwili na ndiyo maana sisi wataalamu, yule tunamuona ni mgonjwa. Kwa wataalamu mtu huyu kumfunga ni kuendelea kumtesa, anatakiwa kutibiwa kwa sababu hamu haiishi,” alisema.
Alisema kwa sababu hamu hiyo huwa inakaa muda mrefu na mtu huyo akitoka ‘soba house’ baada ya muda mfupi na ikiwa hajapata mafunzo stahili, ataanza tena matumizi ya dawa za kulevya.
“Kuna baadhi ya soba house huwa zinatoa mafunzo stahili, kama namna ya kukwepa matumizi ya dawa hizo, kukwepa marafiki wabaya, kufanya kazi halali,” alisema.
Dk Masao alisisitiza kuwa kikawaida arosto haiuwi na kwamba, kibinadamu huwa wanateseka na kuhitaji kupata tiba.