KATIKA miaka ya hivi karibuni mchezo wa soka umekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa nchi zilizopiga hatua zikiwamo zile za barani Ulaya.
Kwa Afrika ambako nchi nyingi ni masikini, soka limekuwa kimbilio la vijana wengi ambao kwao ndicho chanzo kikubwa cha ajira.
Wachezaji, makocha, wauguzi na wafanyakazi wengine wa klabu wamekuwa wakifaidika na utajiri mkubwa unaozalishwa kupitia mchezo huo.
Lakini pia, Serikali kupitia mamlaka za mapato, imekuwa ikinufaika na fedha za kodi zitokanazo na mchezo wa soka.
Pia, klabu zimekuwa zikiingiza fedha nyingi kutokana na mapato ya uwanjani, mauzo ya wachezaji wakiwamo makinda wanaozalishwa katika ‘academy’ zao na hata dili za matangazo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana ya Jarida la Forbes la Marekani, zifuatazo ni klabu ambazo mpaka sasa zimeshavuna fedha nyingi kutokana na biashara ya soka.
Al Ahly (Misri)
Ndiyo timu tajiri zaidi barani Afrika kwa sasa ikiwa na thamani ya euro milioni 19,25. Klabu hiyo ndiyo inayoongoza kwa kuwa na mataji mengi barani Afrika (132).
Lakini pia, inaongoza kwa kutwaa mara nyingi lile Kombe la Klabu Bingwa Afrika ikiwa imefanya hivyo mara nane.
Miaka miwili iliyopita, thamani ya Al Ahly ilikuwa mara mbili ya ile ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Esperance (Tunisia)
Utajiri wao unafikia euro milioni 12,75 na wanamiliki mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hiyo iliyoanzishwa miaka 98 iliyopita, ina heshima kubwa Tunisia ambapo imeshinda makombe 26 ya ligi kuu nchini humo.
Club Africain (Tunisia)
Huenda si mara nyingi umekuwa ukiisikia kwenye mazungumzo ya kila siku, lakini ni moja ya klabu zenye heshima kubwa Tunisia na barani Afrika kwa ujumla.
Wakali hao wanamiliki mataji 13 ya Ligi Kuu Tunisia na utajiri wao unatajwa kuwa ni euro milioni 11, 80.
Mbali na soka, ‘vibopa’ hao wa jijini Tunis, wanamiliki timu za michezo mbalimbali ikiwamo ya mpira wa kikapu.
Uwanja wao wa nyumbani unaoitwa Stade Olympique de Rades, una uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.
Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)
Mamelodi ndiyo mabingwa watetezi wa mbio za kufukuzia taji la ya Mabingwa Afrika mwaka huu.
Walipochukua mwaka jana, ulikuwa ubingwa wao wa kwanza katika historia ya klabu na michuano hiyo.
Mwaka 2001 walikaribia kulitoa mkononi lakini walipochapwa mabao 4–1 na Al Ahly katika mchezo wa fainali. Mamelodi inaongoza kwa kuwa na makombe mengi katika historia ya soka la Afrika Kusini.
Forbes linaitambua klabu hiyo kuwa na utajiri wa euro milioni 10.35.
Kaizer Chiefs (Afrika Kusini)
Kama ilivyo Mamelodi, Chiefs nayo ni miongoni mwa klabu zinazoogelea kwenye dimbwi la utajiri kutokana na biashara ya soka.
Takwimu za kiuchumi za Forbes linaitaja timu hiyo kumiliki utajiri wa euro milioni 10, 48.
Ujenzi wa Uwanja wa Amakhosi unaoingiza mashabiki 55,000 unaomilikiwa na klabu hiyo uligharimu pauni milioni 105.
Mchezo ambao Chiefs huutolea macho zaidi ni ule unaowakutanisha na mahasimu wao wakubwa Orlando Pirates.
Zamalek SC (Misri)
Ilipoanzishwa mwaka 1911, ilifahamika kwa jina la Qasr El-Neel na haikuwa na utajiri iliyonao leo wa euro milioni 10,30.
Mbali na mataji mengine, imeshinda mara tano lile la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Miongoni mwa mastaa wakubwa waliowahi kutamba na timu hiyo ni pamoja na Hassan Shehata, Hossam Hassan, Junior Agogo na Amr Zaki.
Klabu nyingine tajiri
USM Alger (euro milioni 9.65), E.S Setif (euro milioni 8.6), Raja Casablanca (euro milioni 8.13), na T.P. Mazembe (euro milioni 7.70).