Ujanja, na uwezo mkubwa wa kujiongeza kwa Mbunge wa Chalinze, Mh. Ridhiwani Kikwete ndiyo mambo yaliyosababisha kiwanda kipya cha vigae kijengwe Chalinze badala ya Mkuranga mkoani Pwani kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Kikwete akiwa kwenye kipindi cha East Africa Breakfast amesema aliweza kujenga hoja kwa wawekezaji waliokuja nchini kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho, zilizotosha kuwashawishi ni kwanini wajenge Chalinze badala ya Mkuranga.
Miongoni mwa hoja alizojenga ni pamoja na jiografia ya eneo la Chalinze kuwa kitovu cha mikoa karibu yote ya Tanzania kwa kuwa ni njia panda, na pia Chalinze kuwa ni kitovu cha kibiashara kwa kuwa kuna urahisi wa usafirishaji wa bidhaa hiyo kwenda mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi.
Pia amesema Chalinze ni eneo ambapo kuna urahisi wa kupata malighafi kwa ajili ya utengezaji wa bidhaa hiyo, ambapo Chalinze ni katikati ya maeneo yote ambako malighafi hizo zinaweza kupatikana ikiwa ni pamoja na Pugu, Rufiji, Iringa na Morogoro.
"Hawa watu wa Tryphod walipokuja, kwanza walitaka kuwekeza Mkuranga, nikapata fursa ya kwenda kuonana na Meneja Rasilimali Watu wao, nikazungumza nao, na nikamueleza kuwa fursa kubwa za kibishara ziko Chalinze". Amesema Kikwete
Amesema baada ya kuwashawishi, walimuelewa na kukubaliana naye, huku akiungwa mkono pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
Ametaja miongoni mwa manufaa yatakayopatina ni pamoja na fursa ya ajira kati ya 6000 hadi 8000 kwa wakazi wa eneo hilo na nje ya eneo hilo, na tayari ujenzi umekwishaanza.