Kisa cha Kweli:Rafiki Aliyefungwa Miaka 30 kwa "Kubaka",Daftari la Wageni NECTA Likamuokoa Kifungoni..!!!


Huyu ni Rafiki yangu toka udogo,tukiwa shule ya Msingi mpaka Sekondari.Tulikaa pamoja na kusoma pamoja.Namzungumzia rafiki wa kufa na kuzikana.

Duniani kuna visa wakuu,visa hivi visikie kwa jirani lakini visikukute wewe au mtu wako wa karibu.Miaka 10 iliyopita,mwezi kama huu,huyu ndugu yangu alianza taratibu za kukata rufaa ili shauri lake liweze kusikilizwa tena.

Alifungwa kifungo cha miaka 30 gerezani.Kesi yake ilikuwa ya kutungwa na kubambikiwa.Pesa ilitembea na wakubwa wakaisimamia kesi yake.Nakumbuka alivyolia kwa kilio cha nguvu,siku Jaji alipogonga meza baada ya kumuhukumu kutumikia miaka 30 behind the bars!!

Kosa la kusingiziwa kubaka lisikie tu,kweli sio wote walio garezani wana hatia,wengine ni kesi za kusingiziwa.

Kila nilipoenda kumcheki gerezani jamaa alikuwa analia sana.Aliamua kuwa muhubiri na mwimba kwaya wa gerezani,katekista na muongoza ibada mbalimbali mle gerezani.Aliamini ipo siku atatoka,maana alimlilia Mungu wake,toka mawio ya jua mpaka machweo yake.

Baada ya miongozo ya watu wa gerezani(Wafungwa wengi hujua sana taratibu za sheria na namna ya kukata rufaa) jamaa aliamua kukata rufaa.Hoja kubwa ikiwa,siku na tarehe aliyoshutumiwa kutenda kosa,ndio siku na tarehe aliyokuwa Dsm,eneo la baraza la Mitihani akifuatilia "result slip" yake.

Huu ndio ulikuwa ushahidi mkubwa,kitabu cha wageni cha baraza la mtihani,kilionyesha mnamo terehe hiyo,siku hiyo,majira fulani mshitakiwa aliandika jina lake na sahihi yake ktk kitabu cha wageni kwenye lango la Baraza la Mitihani-Dsm.

Kitabu kile kilithibitishwa na Baraza la Mitihani kuwa ni sahihi,na baraza likathibitisha kuwa,tarehe tajwa,na siku tajwa ya mwezi tajwa,majira ya mchana,kitabu kinachoonyesha kuidhinishwa na kutolewa kwa "result slip" kilikuwa na sahihi ya afisa wa NECTA na mchukuaji wa "result slip" ambaye ndio mtuhumiwa.

Ndugu mwema alishinda kesi,sahihi na jina ktk vitabu vya NECTA vilmuokoa kuendelea kutumia miaka 29 iliyobaki baada ya kuwa tayari ametumikia mwaka mmoja jela.Ilikuwa ni siku ya ajabu,ikawa kama ndoto,ilikuwa ni siku ambayo majina na utukufu wote wa Mungu ulitajwa.Siku hii,kwa sahibu wangu,haikuhitaji muujiza wa kuhamisha mlima toka uwanda mmoja kwenda mwingine.Rufaa ile iliyoambataba na ushindi,ulikuwa ni muujiza tosha.

Pesa hudunisha utu,pesa hununua haki na pesa hubadili haki kuwa batili na batili kuwa haki.Sio wote walio gerezani wana hatia,na sio wote hawana hatia.

Sasa ni baba wa watoto watatu,ni miaka kumi na ushee sasa imepita.Kama ilivyo kwa wengine kukumbuka siku yao ya kuzaliwa,kwa ndugu yangu hii ndio siku kubwa ya kukumbukwa maishani mwake.Kila ifikapo,huandaa ibada na sadaka...Kumwambia Mungu...WEWE NI MUNGU WA HAKI.

Imebaki kuwa simulizi,itakuwa historia na baadae hadithi.Kimoja na kikubwa,huwa hatamani kuisimulia hii kwa mke wake,na hadhani kama atakuja kuisema kwa watoto wake.Imebaki kuwa fundo la siri katikati ya mifupa ya kifua chake.

Hii ni habari ya rafiki kipenzi,mjelajela wa kubaka!Ambaye hata kwa uso na sura yake,hudhani kuwa anaweza kutamani kubaka, achilia mbali hata kubaka kwenyewe.Haki mbinguni,duniani ni ubatili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad