Baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platinumz kuonekana kukiuka Sheria za Usalama Barabarani, ametozwa faini ya Sh60,000 katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Usalama Barabarani kwa makosa mawili ya kutofunga mkanda na kuachia usukani wakati akiendesha gari lake akiwa na familia.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema walimuita Diamond baada ya kuona kipande kifupi cha video kwenye mtandao wa Instagram.
“Alitii wito na alikuja juzi ila nilikuwa na kazi nyingi sikuweza kuonana naye na leo (jana) aliweza kufika tena tukaonana, akalipa faini na tukamuonya kufanya kitendo kile alihatarisha maisha ya familia yake,” amesema Mpinga.
Mpinga amesema kutokana na umaarufu wake ndani na nje ya nchi kitendo hicho kingesababisha mashabiki wake kumuiga na kusababisha ajali.