Kutana na Mr Liu Lingchao..Binadamu Konokono Aliyebeba Nyumba Mgongoni Kwa Miaka 5 Akiwa Safarini Kurudi Kijijini Kwake..!!!


ANAITWA Liu Lingchao, raia wa China, ambaye alitembea kwa mguu kwa miaka mitano akiwa na nyumba mgongoni mwake.

Miaka zaidi ya 20 iliyopita, Liu Lingchao aliondoka mji wake mdogo wa nyumbani uliopo katika Jimbo la Guangxi kuelekea majiji makubwa ya ndoto yake Guangzhou na Shenzhenof kutafuta maisha. Naam, alifanikiwa kupata ajira.

Lakini miaka zaidi ya mitano iliyopita mambo yalimwendea vibaya baada ya kufukuzwa kazi na kisha kutimuliwa kutoka nyumba alimokuwa akiishi kutokana na ukosefu wa fedha za kulipia pango.

Hilo lilimfanya achukue uamuzi mgumu kinyume na ule alioufanya zaidi ya miaka 20 iliyopita;- kurudi nyumbani kuliko kuishia kutaabika katika miji ya watu, ambako hakuwa na msaada.

Katika safari hiyo ya kurudi nyumbani, badala ya kuchukua usafiri wa kueleweka, ambao ungemchukua saa zisizozidi 12 iwapo angetumia njia ya barabara kama hapa Tanzania, pengine kutokana na kutokuwa na kitu mfukoni alichagua kutembea maili 450 nzima kurudi nyumbani kwa mguu.

Kichekesho zaidi ni kwamba ili kukabiliana na hali ya hewa kama vile mvua, ilibidi atengeneze nyumba ambayo ataibeba mgongoni kwa safari yake yote hiyo ya mwendo wa konokono.

Utembeaji huo kutoka Shenzhen hadi jimbo la nyumbani la Guangxi ni sawa wa kutembea kutoka New York hadi North Carolina nchini Marekani au karibu sawa na umbali kutoka Dar es Salaam hadi Njombe nchini Tanzania.

Umbali huo si mchezo! Lakini pia mbona kuna simulizi za watu wakitembea maili 3,000 kutoka pwani moja hadi nyingine ya Marekani ndani ya mwaka tu?

Sasa kwanini ilimchukua Liu miaka mitano kutembea moja ya sita (1/6) ya umbali huo?

Pengine ni nyumba hiyo yenye uzito wa kilo 60. Urefu na upana wa futi 5 x 7 iliyong’ang’ania mgongoni mwake ilimchelewesha?

Maswali hayo yanaweza kujibiwa na hili, Liu alikuwa akijitegemea kwa asilimia 100 kwa mahitaji yake ya msingi ya kimwili ikiwamo maji, chakula na kadhalika wakati wa safari hiyo.

Fedha za kujitegemea angezipata wapi ilihali hana ajira wala kipato? Lingchao alikuwa akiokota barabarani makopo na chupa zilizotumika na kuziuza katika miji aliyopitia katika safari yake hiyo ya kurudi nyumbani na hilo lilimwezesha kupata mahitaji yake.

Hivyo, hakuwa katika haraka ya kufika nyumbani mara moja, kwamba ilimbidi ahangaike nyumbani.

Hayo kwa pamoja ni kiini kilichomchelewesha, yaani kilichomfanya achukue miaka mitano kuwasili nyumbani.

Muuzaji huyo (38), alijiwa na wazo la kuwa na nyumba hiyo aliyoitengeneza kutokana na mianzi na plastiki ili kukabiliana na changamoto ya hali ya hewa wakati wa safari yake hiyo ya miaka mitano.

Anasema nyumba yake hiyo inamfanya kuwa huru na anaibeba kila aendako kusini mwa China wakati akiuza chupa za vinywaji anazoziokota barabarani.

“Nilichoshwa na matukio ya mara kwa mara ya kujikuta nikinyeshewa na mvua mithili ya kuku nisiye na makao maalumu.

“Hata nilipoona mahali pakavu kama vile chini ya daraja, au katika jengo lililotelekezwa nilikuta tayari kuna mtu ameniwahi kujihifadhi na ilinibidi niombe ruhusa ya kuchangia kujihifadhi.

“Ikaja siku nilipochoshwa na hali hii nikaamua kujenga nyumba yangu kutokana na mianzi katika shamba moja nilililopata kibarua cha wiki kadhaa.

“Wakati kazi ilipoisha na hivyo vibarua kutawanyika, wakati wa kuhama niliona vyema nihame na nyumba hiyo na hivyo nikairekebisha ili iniwie rahisi kuibeba na tangu hapo sikurudi nyuma,” anaeleza.

Akipewa jina la ‘Konokono Mkubwa wa Kibinadamu,’ nchini humo, Lingchao alitembea maili 20 kwa siku 20 na alitumia nyumba tatu alizozitengeneza na kuzibeba mgongoni baada ya mbili za awali kubomoka.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad