Baada ya kukaa mahabusu kwa siku nne, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema kuwa maneno anayoshtakiwa kwa kuyatamka ni ya kweli na kuwa siyo kosa.
Lissu ambaye yupo nje kwa dhamana, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka manne ya kutoa maneno ya uchochezi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa.
Awali, kabla ya kupandishwa kizimbani mbunge huyo aligoma kula akiwa mahabusu ya polisi kwa mujibu wa wakili wake, Peter Kibatala.
Kutoka kwa Lissu kulifuatia kasoro za kuandaa kiapo kuwa mojawapo wa sababu zilizoifanya Mahakama hiyo kutupa pingamizi la dhamana lililowekwa na upande wa Serikali.
Mbunge huyo amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka manne ya kutoa kauli za uchochezi, ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha ombi la zuio la dhamana lililoambatana na kiapo cha Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilaya Ilala, Mrakabu Msaidizi (ASP), Denis Mjumba.
Hata hivyo, mahakama hiyo imetupa pingamizi la dhamana pamoja na mambo mengine kutokana na kasoro katika kiapo hicho.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo, Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi ameainisha mambo matatu yaliyomfanya kulikataa pingamizi hilo na kuamua kumwachia kwa dhamana mtuhumiwa.
Lissu ametimiza masharti hayo na kudhaminiwa na Diwani wa Kata ya Tabata wa chama hicho, Patrick Asenga hivyo akaachiwa huru.