Rais John Magufuli amefichua sababu za kumuongezea siku nne zaidi aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, akisema kwa kuwa alikuwa nje ya nchi, hakuwa na mtu anayemwamini kumwachia nafasi hiyo.
Mwamunyange alistaafu rasmi Januari 31, 2017 na alimtaarifu Rais Magufuli wakati akijiandaa kusafiri kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU).
Akizungumza wakati wa hafla ya kumwapisha mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Venance Mabeyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema alipata wakati mgumu kuteua mrithi wa Jenerali Mwamunyange ndani ya siku nne ambazo alisafiri kwani alikuwa bado hamjui.
“Nilipokuwa nikienda kwenye mkutano wa AU, Jenerali Mwamunyange aliniambia ‘unajua siku zangu zinaisha tarehe 31 (Januari), sasa ninafanyaje, naomba umteue anayekuja’. Nikasema ‘sasa nikiondoka leo nikamteua (mkuu mpya) tarehe 24 (Januari) na wewe unaondoka tarehe 31 (Januari), si wataanza kusema nimekutumbua? Kwa sababu Watanzania wanajua kubadilisha maneno kweli. Wataanza kusema fulani ametumbuliwa kabla ya wakati wake na hiyo ndiyo itakuwa stori’,” alisema Rais.
“Lakini nikamwambia mimi nasafiri, ninayekujua ni wewe, ninayemteua simjui. Sasa nikishamteua ambaye simjui, hizi siku nne ambazo nitakaa nje itakuwaje?”
Alisema ilibidi amwombe Jenerali Mwamunyange aendelee na wadhifa huo hadi atakaporudi kutoka Ethiopia.
Rais Magufuli alisema akiwa Ethiopia, viongozi wa nchi nyingine walikuwa wakiulizia nani anayerithi baada ya Mwamunyange kuondoka.
“Nikawa naulizwa nani atakuwa mkuu wa majeshi, naulizwa na watu wa nchi nyingine, wala si Watanzania. Nikajua kumbe hii nafasi inaangaliwa na watu wengi,” alisema Rais Magufuli.