RAIS John Magufuli juzi aliwaeleza rasmi mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa azma ya serikali kuhamishia Makao Makuu mjini Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake na kuwaomba nao waanze mchakato wa kuhamia Dodoma.
“Mwaka jana wakati nakabidhiwa uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi niliahidi ndani ya miaka mitano serikali itahamia Dodoma," taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilisema juzi.
"Tayari Waziri Mkuu na baadhi ya wizara zipo Dodoma. Nawaomba mabalozi nanyi muanze kufikiria kuhamia Dodoma kwani serikali imekwishatenga viwanja kwa ajili yenu."
Kwa upande wake, taarifa ya Wizara ilisema juzi, Kaimu Mkuu wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe nchini, Edzai Chimonyo alisema Jumuiya ya Mabalozi inaunga mkono wazo hilo na wapo tayari kuhamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Taarifa hiyo ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilisema Rais Magufuli alitoa taarifa hiyo wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya.
Hafla hiyo, imeelezwa, ilifanyika Ikulu, Dar es Salaam kati ya Rais, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini.
Rais Magufuli, imeelezwa pia, alitumia hafla hiyo kuwashukuru mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kwa ushirikiano na mchango wao kwa serikali ambao umesaidia kufikia malengo ya mwaka uliopita.
Aidha, Rais Magufuli amewasihi mabalozi hao kuendelea kuisaidia Serikali ili kufikia malengo iliyojiwekea kwa mwaka huu.
Katika hotuba yake, imeelezwa, Rais Magufuli alisema mwaka 2016 ambao ulikuwa mwaka wake wa kwanza madarakani umekuwa wa mafanikio makubwa ambapo nchi imendelea kudumisha amani, mshikamano, umoja na muungano umeimarika.
Aidha katika mwaka huo, taarifa ya Wizara ilisema, Rais Magufuli alisema serikali imeongeza jitihada za kuimarisha demokrasia, kupiga vita rushwa, ujangili na ufisadi.
Akizungumzia suala la ukusanyaji mapato, Rais Magufuli alisema serikali inasimamia kikamilifu ambapo kwa sasa kiwango cha ukusanyaji wa mapato kimeongezeka kutoka Sh. bilioni 850 hadi kufikia Sh. trilioni 1.2 kwa mwezi, taarifa ilisema.
Kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016-2021, taarifa ilisema Rais Magufuli aliwaeleza mabalozi kuwa mpango huo unalenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyoelekeza.
Rais Magufuli alisema kwenye hafla hiyo kuwa katika kutekeleza mpango huo, Sh. trilioni 107 zinahitajika na kati ya hizo serikali itatoa Sh. trilioni 59 ambazo ni wastani wa Sh. trilioni 11.8 kila mwaka, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Taarifa ilisema Rais aliwaambia wageni wake kuwa utekelezaji wa mpango huo umeshaanza ambapo serikali katika bajeti yake ya mwaka 2016 imetenga kiasi cha Sh. trilioni 29.5, sawa na asilimia 40 ya bajeti ya serikali, kwa ajili ya maendeleo.
Ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kutengwa kwenye bajeti ya maendeleo katika historia ya Tanzania.
Fedha hizo, alisema Rais Magufuli, zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kama vile nishati, barabara, reli na maji.
“Hii imetuwezesha kuendelea au kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga, maji pamoja na miradi ya umeme," taarifa ya Wizara ilimnukuu Rais. "Tuliweza pia kununua ndege mpya sita ambazo bila shaka zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini.”