“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha katika kipindi hiki cha masika hamtakiwi kujipa ujasiri na kuyakadiria maji ya mvua hivyo zinahitajika tahadhari za kutosha dhidi ya watoto, au vyombo vyovyote vya usafiri kwani maji hayo huwa yanakwenda kwa kasi, yasubirini yapite acheni hisia ili kuhakikisha maisha yenu hayahatarishwi na mvua”. Alisisitiza Kamanda Mkumbo.
Kamanda Mkumbo alitoa wito huo baada ya jana usiku kunyesha mvua kubwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu na kusababisha vifo vya watu saba. Alisema katika tukio la kwanza jana Usiku wa saa 4:00 katika kijiji cha Kimbolo kata ya Enaboishu wilayani Arumeru, watu watano wote wakazi wa kijiji cha Kyoga walifariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Premio lenye namba za usajili T 579 BSG kusombwa na maji.
Akiwataja watu hao waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Shengai Saiguran (30), Nembris Mungaya (20), Minis Loyi (25), Inoti George (40) na Ngaisi Moluo ambaye umri wake bado haujafahamika mara moja huku dereva wa gari hilo Yusuph Jacobo akinusurika.
Kamanda Mkumbo alisema mbali na vifo vya watu hao pia watu wengine wawili walifariki dunia katika maeneo tofauti ambapo katika kijiji cha Keriani mtu aitwaye Babu Robikeki alisombwa na maji kisha kufariki dunia wakati anavuka mto wakati akitokea matembezini.
Wakati mtu wa saba ni Seuli Meseyeki (37) dereva wa boda boda ambaye alikuwa anaendesha pikipiki aina ya T-Better yenye namba za usajili T. 726 DFD naye alisombwa na maji eneo la Olorieni Ngaramtoni wakati anavuka barabara. Pia pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 892 ACR iliokotwa maeneo ya Olasiti kwa Mawala halmashauri ya jiji la Arusha huku dereva wake hajulikani alipo.