SIKU chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutaja watuhumiwa 65 katika vita dhidi ya dawa za kulevya, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema haki zimekiukwa katika utajaji majina.
Mbali na LHRC baadhi ya wanaharakati wameungana na kituo hicho kukosoa utaratibu uliotumiwa na Makonda.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kutangaza majina ya watu kwa kuwahusisha na dawa za kulevya bila uchunguzi, ni kinyume na haki za binadamu na kuchafua majina yao kwa vile hakuna uthibitisho wa kuwahusisha na tuhuma hizo.
Alisema hayo baada ya mwandishi wa habari hizi kumtaka azungumzie mazingira ya kutaja majina ya watuhumiwa kwa kulinganisha na misingi ya haki za binadamu.
Dk Bisimba alisema majina ya watu yalipaswa kutajwa kama Jeshi la Polisi nchini lingefanya uchunguzi wa awali na kupata uthibitisho na Mahakama ndiyo yenye jukumu la kutoa haki kwa kutafsiri sheria na si kiongozi.
“Kama uchunguzi wa awali ungefanyika, suala la kutaja majina lingekuwa sahihi, lakini kutangaza bila upelelezi ni kinyume na sheria,” alisema.
Alisema Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema walipata kupokea majina ya uongo, hivyo ni hatari kutangaza jina la uongo kisheria.
Wakili wa Kujitegemea, Nassor Kitugulu alisema ni jambo la kushangaza mtu kutaja mbinu za adui, hiyo ni dalili kuwa vita hiyo ni ngumu bila ushirikiano.
Alisema iwapo Serikali imedhamiria kupambana na dawa za kulevya nchini baada ya kutambua njia zinazotumiwa, ilipaswa kuweka mitego ya kunasa watuhumiwa.
“Tunajua kuwa dawa za kulevya zinapoteza nguvukazi, lakini utaratibu wa kutangaza bila uthibitisho wa tuhuma ni kuchafua sifa ya mtu kwenye jamii,” alisema.
Naye Fidelis Butahe anaripoti kutoka Dodoma, kwamba Bunge juzi usiku liliweka historia kwa kupitisha maazimo manne, yakiwamo ya kumtaka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na ikibainika wana makosa mamlaka zao za uteuzi ziwawajibishe.
Wateule hao wa Rais wanadaiwa kutoa kauli za kudharau Bunge takribani siku tatu zilizopita na kuamsha hisia za wabunge waliotoa kauli za kuwakemea bungeni.
Kwa sakata hilo, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) aliwasilisha hoja ya kutaka washughulikiwe, ambayo ilijadiliwa kuanzia saa 1.30 usiku hadi saa 2.15 usiku na kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema “ndiyo”.
Wakati wa mjadala wa hoja hiyo, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya (Chadema) alieleza jinsi Makonda alivyompigia simu kumweleza kuwa atawashughulikia wabunge, kwa sababu yuko karibu na ‘Bwana mkubwa’, huku Joseph Msukuma (Geita Mjini-CCM) akitangaza vita na Mkuu huyo wa mkoa.
Ilikuwa kama sinema bungeni, kutokana na wawakilishi hao wa wananchi kuonekana kama wabunge wa chama kimoja, walipotoa hoja zao kupinga kauli hizo, huku Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akiwaongoza kufuata kanuni za chombo hicho katika mjadala huo.
Maazimio hao ni; Makonda na Mnyeti kuitwa mbele ya Kamati, Waziri wa Tamisemi kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya namna ya kufanya kazi zao bila kuingilia mihimili mingine.
Pia, mamlaka nyingine zikimhitaji Mbunge kwa mashitaka ya aina yoyote lazima zimjulishe Spika wa Bunge na mamlaka ya kinidhamu kuwawajibisha wateule hao wa Rais ikibainika wametenda kosa la kudharau chombo hicho.
Ilivyokuwa
Akiwasilisha hoja hiyo usiku baada ya kipindi cha asubuhi kutoruhusiwa na Chenge kwa maelezo kuwa alitaka kujiridhisha kama Mbunge huyo alizingatia kanuni, Waitara alisema Mnyeti ameonekana katika mitandao ya kijamii akisema wabunge hawajielewi.
“Haya mambo ndiyo yamejirudia wakati nikiangalia televisheni ya Clouds, Makonda akionekana akisema sisi humu bungeni tunasinzia,” alisema Waitara.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63(2), Bunge ndicho chombo kikuu kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na linapitisha bajeti inayotumiwa na wateule hao wa Rais.
Alisema si sawa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka rumande wabunge, madiwani na watumishi wa Serikali.
“Bunge linaingia katika majaribu makubwa ya kudharauliwa. Tunakula kiapo humu, tuamue kwa niaba ya Watanzania, lakini Mkuu wa Wilaya anasema hawa ni wapuuzi na Mkuu wa Mkoa anasema hawa wanalala tu,” alisema.
Baada ya hoja hiyo, Waitara alitaka ijadiliwe na Bunge na kutoa maazimio ili kurejesha heshima ya chombo hicho, hoja ambayo Chenge aliipokea na kutoa nafasi kwa wabunge wanne, kujadili kutokana na ufupi wa muda.
Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu alisema: “Nimehuzunika sana wabunge tunafika mahali tunadharauliwa, halafu watu tunaangalia tu. Haya ambayo yametokea kwa Makonda na Arumeru, pia yametokea Manispaa ya Dodoma. Mkurugenzi anaongea na wabunge kama watoto.
“Mimi nadhani hata ile sheria ya Marekani wenzetu wanaoteuliwa kwa ngazi za juu lazima wapelekwe bungeni, hapa kwetu ingefaa kuletwa ili watu wa aina hii tuweze kuwamaliza hapa hapa. Wapo wanaodhani wako juu yetu.”
Alisema ni jambo la hatari kujenga Serikali yenye kiburi na kusisitiza: “Unapotaka kutoa pepo halibembelezwi. Unataka kupunga majini huwezi kubembeleza. Lazima ukazane kupunga jini litoke. Hatuwezi kutoa pepo kwa lugha nyepesi nyepesi (akipunguza sauti) pepo toka, haiwezekani. Kama ni pepo tulikemee litoke.”
Bulaya alibainisha jinsi Makonda alivyompigia simu na kutamba kushughulikia wabunge kwa kuwa yeye yuko karibu na ‘Bwana mkubwa’, huku akisisitiza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa hakutengezwa kuwa kiongozi.
“Makonda alinipigia simu na kunitisha kwamba yeye yuko karibu na Bwana mkubwa, atatushughulikia wabunge. Alisema ataanza na Msukuma, Halima Mdee (Kawe-Chadema), Esther Matiko (Tarime Mjini-Chadema), Sugu (Joseph Mbilinyi-Chadema Mbeya Mjini) na Msigwa (Mchungaji Peter-Iringa Mjini-Chadema),” alisema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema: “Ni lazima heshima ya Bunge ilindwe kwa gharama yoyote. Makonda anawapigia simu wabunge akitaja mmoja wa mawaziri kuwa ndiye anatuma wabunge wamtukane.”
Naye Msukuma alisema haiwezekani Makonda afanye kazi ya polisi na kuhoji aliko Mkuu wa Jeshi la Polisi, makamanda na makamishna wake.
“Makonda ni nani katika hii nchi? Kama Jairo (David-aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini) alitoka kwa azimio la Bunge, Makonda ni nani? Mimi niko tayari kupambana na Makonda,” alisema Msukuma.
Hoja hiyo pia ilitolewa ufafanuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakitaka wahusika hao wasikilizwe kwanza na kuachia ngazi zingine iwapo watabainika kutenda kosa.
Chenge
Baada ya wabunge kuchangia, Chenge alitoa nafasi kwa Waitara ambaye alihitimisha hoja hiyo na kutoa maazimio manne ambayo Mwenyekiti huyo wa Bunge aliyafafanua na kupitishwa.
“Ni kwamba Waziri wa Tamisemi atoe waraka kwa wahusika (wakuu wa mikoa na wilaya) kuwaeleza namna ya utekelezaji wa majukumu yao. Pili, wahusika waitwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,” alisema Chenge.
“Endapo itaridhika, baada ya Kamati kuwasilisha taarifa bungeni na Bunge kuridhia kwamba kuna jinai, hasa sheria yetu ya Bunge inatoa madaraka kwa AG kufuatilia na vyombo vingine vya Dola,” alisema Chenge.
Alisisitiza: “Sisi hatuwezi kufika huko tunaishia katika haya yatakayoletwa na Kamati na suala la uwajibikaji linakwenda sambamba na hayo yatakayoletwa na Kamati.”
Alipolihoji Bunge kama linakubaliana na hoja hiyo, hali ilikuwa hivi; “mnaokubali hoja hii semeni ndiyo.” Wabunge wote waliitika “ndiyo” na aliposema wasiokubaliana na hoja hiyo waseme “siyo”. Bunge lilibaki kimya.