WATENGENEZAJI wa vileo vinavyofungashwa kwenye 'viroba' ambavyo vimepigwa marufuku kuanzia mwezi ujao, wamepewa wiki moja kuomba kibali cha muda cha kuendelea kuzalisha, wakati wakitafuta teknolojia ya kuviweka kwenye chupa.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Luhaga Mpina, aliliambia gazeti dada la The Guardian katika mahojiano juzi kuwa ili kupata kibali cha muda, mtengenezaji atahitaji kutimiza masharti kadhaa kabla ya Jumanne ijayo.
Mpina alisema watengenezaji hao watatakiwa kuwa na cheti kinachoonyesha kuwa hawana deni la kodi kwa miaka mitatu mfululizo iliyopita kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA).
Aidha, Mpina alisema, mtengenezaji wa viroba ambaye hana uwezo wa kuweka kilevi kwenye chupa kwa sasa atalazimika kuwa na barua ya kumruhusu kukitengeneza kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Mbali na vibali hivyo viwili, cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango la Taifa (TBS) na hati ya tathmini ya uharibifu wa mazingira kutoka Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) vitahusika, alisema Mpina.
Takwa jingine ni barua ya dhamana kuwa mtengenezaji hatotumia teknolojia bandia, na barua ya usajili wa biashara kutoka Mamlaka ya Usajili wa Biashara (BRELA) inayothibitisha usajili wa kampuni na umiliki wa jina la kileo.
Mpina alisema serikali itafikiria kutoa nyongeza ya muda wa uzalishaji viroba kwa maombi ambayo yatakidhi matakwa yote.
“Serikali inakusudia kutekeleza kifungu cha 14 cha Katiba ambacho kinatoa haki kwa wananchi kuishi katika mazingira safi, salama na ya afya,” alisema.
Pia alisema lengo ni kudhibiti uharibifu wa mazingira unaochangiwa na viroba vilivyotumika, pamoja na kukomesha ukwepaji kodi unaotokana na teknolojia dhaifu ya upakiaji hiyo, ambayo husababisha serikali kukosa Sh. bilioni 600 katika mapato kwa mwaka.
MACHI MOSI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wiki iliyopita kuwa kuanzia Machi mosi serikali itapiga marufuku pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.
Alitoa kauli hiyo Februari 17 wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.
“Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika," alisema.
"Sasa hivi viroba vimeenea kila kona; hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo.
"Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”