Video Queen mwenye umbo ‘matata’ Bongo, Agnes Gerald ‘Masogange’, amesoteshwa rumande na Jeshi la Polisi kufuatia kuendelea kumshikilia katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ‘Central’ kwa msala wa madawa ya kulevya huku ndugu zake nao wakisota kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakisubiri apandishwe kizimbani bila mafanikio.
Februari 16, mwaka huu, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Simon Siro, lilithibitisha kumshikilia mrembo huyo kwa mahojiano na vipimo juu ya tuhuma za kujihusisha na utumiaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya huku likiahidi kumfikisha mahakamani jana lakini likagonga mwamba.
Mapema jana, Risasi Jumamosi liliweka kambi mahakamani hapo likimsubiria Masogange endapo atafikishwa na kupandishwa kizimbani kusomewa mashitaka yake lakini hadi mawio, mrembo huyo hakufikishwa kwa madai ya kutokamilika kwa upelelezi wa mashitaka yake.
Ndugu, jamaa na marafiki wa Masogange walijitokeza mahakamani tangu asubuhi wakisubiria kama ndugu yao huyo atafikishwa mahakamani hapo lakini hakuweza kufikishwa hivyo wakajikuta wakikata tamaa baada ya kusota kwa muda mrefu hivyo kuondoka eneo hilo kwa huzuni na kulengwalengwa na machozi.
Wakiwa kwenye banda la kusubiria, ndugu hao wa Masogange, muda mwingi walisikika wakinung’unika kutokana na ndugu yao kukawizwa kufikishwa mahali hapo kiasi cha wengine kuamua kwenda Central kuulizia kama uwezekano wa kumleta utakuwepo.
Baadhi ya waliokwenda Central waliulizia kwa askali waliokuwepo kituoni hapo na kujibiwa kuwa hataweza kufikishwa mahakamani jana kufuatia majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali kukawia kufika polisi.
Baada ya hali kuwa hivyo, waliporudi Kisutu walikusanyana pamoja na kuamua kuondoka mahakamani hapo huku wakilalama kuwa, ni kwa nini kama polisi walifahamu wazi kwamba jana hawatamfikisha, wangewaambia ili waendelee na shughuli zao.
“Hatujapendezwa kabisa na hali hii, maana kama walijua hawataweza kumfikisha mahakamani leo (jana) hapakuwa na sababu ya kutuficha, maana tungewaona wema kama wangesema tukaendelea na shughuli zetu.
“Hebu ona sasa hawajamleta na leo (jana) ni Ijumaa, kama siyo usumbufu ni nini? Kutomleta maana yake si watamuweka hadi Jumatatu?,” walisikika wakilalama baadhi ya ndugu hao.
Hadi Risasi Jumamosi linaondoka mahakamani hapo majira ya saa 10:00 jioni, Masogange alikuwa hajafikishwa kwa madai ya kutokamilika kwa baadhi ya nyaraka za upelelezi wa kesi yake hiyo.