Baada ya kuwepo kwa dhana ya huenda wabunge wanapingana na vita dhidi ya dawa za kulevya iliyoasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, mmoja kati ya wabunge wa bunge hilo ameibuka na kutoa ufafanuzi kuwa dhana hiyo siyo ya kweli.
Mbunge huyo ni Elibariki Kingu, wa Singida Magharibi, ambaye alikuwa kwenye kipindi cha East Africa Breakfast, cha EA Radio ambapo amesema kuwa wabunge wote kwa ujumla wanaunga mkono vita hiyo, lakini hawakubaliani na njia anayoitumia Makonda ya kutaja majina ya watu hadharani bila kuwa na ushahidi wa kutosha.
Pia Kingu amesema suala lingine ambalo ndilo lililowakwaza wabunge ni kauli iliyotolewa na makonda inayoonesha dharau na kushusha hadhi ya Bunge.
Pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi alioufanya wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Dkt. Rogers Sianga, huku akimshauri kushulikia majina ya wote waliotajwa.