Mbwa Wakamata 20 Dawa za Kulevya...!!!


WATU 20 wamekamatwa kwa msaada wa mbwa wa polisi mkoani hapa katika wiki moja iliyopita, wakituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Watu hao walikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kuanza kutumia mbwa maalumu ili kusaka watuhumiwa wa madawa hayo, kwenye mabasi yanayopita barabara kuu zinazoingia na kutoka mkoani Singida.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Debora Magiligimba alisema njia hiyo imesaidia kukamata watuhumiwa 20 ambao walikutwa na zaidi ya misokoto 7,000 ya bangi, 'unga' aina ya heroine na mirungi. Alisema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu ili kukabiliana na wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya.

Kamanda Debora alisema wauzaji na watumiaji wamekuwa wakibuni njia mpya kila siku kwa ajili ya kufanikisha "shughuli zao haramu".

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini imepata msukumo mpya tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ataje watu 65 waliotakiwa kuisaidia polisi kuhusu biashara ya mihadarati wiki mbili zilizopita.

Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa na viongozi wa dini, wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya polisi 12 na wasanii kadhaa ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Vita hiyo ikaongezwa nguvu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Manguvita ambaye naye aliamuru katika taarifa Makamanda wa mikoa yote nchini waongeze nguvu.

Tangu hapo, zaidi ya watu 500 wamekamatwa katika mikoa mbalimbali nchini wakihusishwa kwa namna moja au nyingine na biashara ya dawa za kulevya.

Katika matukio yote hayo ya ukamataji, hata hivyo, makamanda wa polisi wa mikoa walielezea kukamata watuhumiwa bila ya kuhusisha mbwa waliopewa mafunzo maalumu ya kugundua mihadarati.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Masauni alikabidhiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser mbwa maalumu wa kubaini madawa ya kulevya na pembe za ndovu mwaka jana, tukio lililofanyika kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

ZOEZI ZURI

Abiria wa mabasi yaliyofanyiwa upekuzi kwa kutumia mbwa wa polisi na kuzungumza na Nipashe, walieleza kufurahishwa na zoezi hilo kwa madai kuwa litaondoa uwezekano wa kusambazwa ovyo kwa madawa hayo.

"Zoezi hili ni zuri sana, naomba liendelee ili kupiga vita uuzaji na matumizi yake," alisema, Keneth Paul, abiria raia wa Marekani, aliyesafiri na moja ya basi kutoka Arusha kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa.

"Mimi nilikuwa mtumiaji sana, lakini niliachana nayo na sasa nahubiri injili. Awali akizungumza zaidi, Kamanda Debora alisema mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa na kete moja ya heroine, baada ya upelelezi alibainika kuwa ni mtumiaji, lakini anaendelea na mahojiano zaidi ili kubaini alikoinunua.

Alisema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kamanda huyo wa polisi wa mkoa aliwataka wakazi wa mkoa wa Singida kuendelea kushirikiana na jeshi lake ili kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano katika kutokomeza madawa ya kulevya nchini.

Rais wa tano, John Magufuli ameshaagiza vita hiyo isiache mtu yeyote. “Hakuna mtu maarufu, mwanasiasa, waziri au kiongozi yeyote au mtoto wa fulani, askari ambaye anajihusisha na dawa za kulenya aachwe, hata awe mke wangu Janeth... kamata wote weka ndani,” alisema Rais Magufuli mwanzoni mwa mwezi.

Aidha, Rais Magufuli pia ameshamteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya na kuweka msimamo wa Serikali yake juu ya zaidi ya Watanzania 1,000 waliofungwa au kuhukumiwa kunyongwa katika magereza mbalimbali duniani.

Rais Magufuli amesema serikali haitajishughulisha na Watanzania waliokamatwa ughaibuni na kuhukumiwa kunyongwa kutokana na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad