Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi ambaye amekubali nchi hiyo kuja kujenga viwanda vya dawa nchini.
Katika mazungumzo hayo ambayo ni kando ya Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika uliomalizika jana Mjini Addis Ababa Nchini Ethiopia viongozi hao wamezungumzia namna nchi hizo zitakavyoshirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo na viwanda.
Pamoja na kukubali mwaliko wa Rais Magufuli wa kufanya ziara rasmi nchini Tanzania, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi pia amekubali ombi la kuwaleta wataalamu na wawekezaji wa Misri nchini Tanzania ili wajenge viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba vya binadamu, kuinua teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji, kuwekeza katika viwanda vya nyama na viwanda vingine ambavyo nchi hiyo imepiga hatua kubwa.
“Mhe. Rais El-Sisi nakupongeza sana kwa juhudi zako za kuijenga Misri na nitafurahi sana kuona biashara ya Tanzania na Misri inaongezeka maradufu kwa manufaa ya pande zote mbili” amesisitiza Mhe. Dkt Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli pia amekutana na amekutana na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambapo viongozi hao wamezungumzia miradi mbalimbali ya ushirikiano na fursa za biashara ambazo Tanzania na Uganda zinaweza kuzitumia kujiongezea mapato. Mhe. Rais Museven amekubali kufanya ziara nchini Tanzania katika siku za karibuni.