WAKATI kikosi cha Simba, kesho Jumamosi kikitarajiwa kushuka uwanjani kucheza dhidi ya Prisons ya Mbeya katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, nahodha wa Simba, Jonas Mkude ametoa kauli kuhusu nidhamu yake.
Mkude amesema kuwa yeye siyo mtovu wa nidhamu kama anavyodaiwa kauli ambayo inaweza kupokelewa kwa hisia tofauti na wenzake na mashabiki wa soka ambao mara kadhaa wamekuwa wakimlaumu kuwa ni mtovu wa nidhamu.
Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kuwa kuna baadhi ya wachezaji wenzake wa Simba wamemuomba kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog kumpokonya Mkude unahodha kutokana na nidhamu yake kuwa mbaya.
Mkude hakusafiri na timu yake kwenda Songea kucheza dhidi ya Majimaji na inaelezwa kuwa wenzake hawakufurahishwa na kitendo hicho.
“Mimi siyo mtovu wa nidhamu kama inavyodaiwa na sijui ni kwa nini nimekuwa nikiandamwa na tuhuma hizo kila wakati.
“Ninapokuwa sionekani katika timu siyo kwamba ninafanya kusudi ila ninakuwa na matatizo na huwa natoa taarifa kwa viongozi wangu ambao nawajibika kwao kila siku ambao ni kocha pamoja na meneja, lakini haya ambayo yamekuwa yakisemwa kuwa sina nidhamu ninafanya mambo kwa kujiamulia siyo kweli.
“Kama kuna jambo lolote baya ambalo nililifanya na halikuwapendeza na hiyo ndiyo ikawa sababu ya kusemwa vibaya kila simu basi naomba wanisamehe,” alisema Mkude.