Mvua Kubwa Yaangamiza Maisha ya Watu 4


WATU wanne wakiwamo watatu wa familia moja ambao ni wakazi wa Kijiji cha Isighu kitongoji cha Majumba Sita wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wamekufa maji baada ya makazi yao kusombwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Januari 31.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wilayani hapa, Dk Said Mawji amekiri kupokea miili ya watu wanne na majeruhi wawili.

Dk Mwaji aliwataja waliokufa kuwa ni Maritha Mabula (60), Shukuru Donald (15) mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwana Kianga na Bernadeta Mabula(7) mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Ilolo na mwingine ni Jeska Lubeleje (19) mkazi wa Kijiji cha Chinyika katika Kata ya Vighawe.

Aliwataja majeruhi wawili waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni Beka Mlami na Joseph Sumisumi. Aidha, alisema kwamba majeruhi wametibiwa na kuondoka.

Alieleza kuwa katika ajali hiyo, mmoja wa watoto walionusurika na kifo Beca Mrami (10), alisema maji yaliingia ndani ya nyumba na akalazimika kukimbilia darini na ndugu yake, lakini walipoona yamezidi walikimbia wakimwacha bibi yao na dada zake.

“Mimi nilipoona maji yanazidi nikawaambia tukimbie, lakini bibi na akina dada walibaki ndani; mimi na Mandili (Joseph Sumisumi ) tulipanda juu ya paa baada ya nyumba kuanguka nilikimbia na kuwaacha ndani,” alieleza mtoto huyo.

Mzee wa kaya hiyo, Mabula Sumisumi, alisema hakuwapo katika mji huo siku hiyo alienda kulinda mifugo kambini ndipo alipoambiwa familia yake imesombwa na maji.

Hata hivyo, Sumisumi alisema kila kitu kilichokuwamo ndani kimesombwa na maji ikiwamo akiba ya chakula na fedha kiasi alizokuwa amehifadhi ndani ya nyumba ambazo hakuzitaja kiasi chake.

Shuhuda wa tukio hilo, Simon Kazimoto alisema nyumba hiyo imesombwa kutokana na kuwa ilijengwa kwenye mkondo wa maji na kutokana na uharibifu wa mazingira unaoendelea umesababisha maji kutawanyika na kuingia katika makazi ya watu na kusababisha vifo.

Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Said Kilungo alisema kwa hatua za awali zilizochukuliwa na serikali ni kuhifadhi maiti kwa kugharamia jeneza na sanda kwa kila maiti baada ya hapo hatua zaidi zitafuata. Kilungo aliwataka wananchi wa kitongoji hicho kuhama katika maeneo hatarishi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa.

Pamoja na mvua hiyo, kusababisha vifo vya watu wanne, lakini tayari baadhi ya miundombinu ya Wilaya ya Mpwapwa iko hatarini kusombwa na maji, ikiwamo daraja la Tanesco na daraja la kwenda Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad