NEW DELHI, INDIA: WANAWAKE wawili, Mzambia Thelma Mkandawire (38) na Mtanzania Pamela David Kiritta (41) wamekamatwa kilo nne za madawa ya kulevya (cocaine) yenye thamani ya Rs milioni 300 sawa TZS bilioni 9.7 katika hoteli moja karibu na uwanja wa ndege wa New Delhi nchini India.
Askari wanaohusika na kupiga vita madawa hayo nchini humo (NCB), waliwatia mbaroni baada ya kudokezwa na hivyo kuanza kumfuatilia Mkandawire aliyetua nchini humo kutokea Sao Paulo (Brazil) kupitia Addis Ababa (Ethiopia) ambapo walimvamia akiwa hotelini eneo la Mahipalpur akiwa na Kirrita aliyedaiwa kwenda kuupokea mzigo huo.
Mkurugenzi wa NCB wa Kanda ya Delhi, Madho Singh, alisema madawa hayo yalipatikana katika mizigo ya Thelma na hivyo wanawake wote wawili wamekamatwa kuhusiana na madawa hayo ambayo thamani yake katika soko ni kubwa.
Habari nyingine zilisema kwamba Thelma aliwahi kukamatwa nchini Pakistan mwaka 2015 akiwa na madawa ya kulevya lakini aliweza kuachiliwa kwa madai ya kutoa hongo. Pia habari zimesema Kiritta alikuwa akikaa katika nyumba moja eneo la Vasant Kunj la Delhi Kusini tangu aingie nchini India mwanzoni mwa Januari mwaka huu.
Pamela ambaye hiyo ilikuwa ni safari yake ya tisa kwenda India, alikuwa aupokee mzigo ambapo walivamiwa na askari na kupekuliwa begi lao walikokuwa nalo na kukutwa na madawa hayo waliyokuwa wameyaweka kitaalam kiasi kwamba mashine za uchunguzi zilishindwa kuyagundua kutokana na kufungwa kitaalam.
Inasemekana madawa hayo yangefungwa katika paketi ndogondogo na kusambazwa kwa watumiaji nchini India.
Alipoulizwa, Kiritta alikiri kuingia nchini India mara tisa tangu 2006 na amewahi kwenda katika nchi nyingine za Ecuador na Kenya kwa shughuli kama hizo.