Mchungaji wa Kanisa la Maombezi GRC la jijini Dar es salaam, Anthony Lusekelo maarufu kama 'Mzee wa Upako' ametema cheche kwa Nabii maarufu kutoka Nigeria TB Josua wa Kanisa la SCOAN kuwa ni tapeli na kusisitiza kuwa hapaswi kuaminiwa kwa lolote.
Mch. Lusekelo amesema kuwa Nabii TB Joshua ni tapeli kwani alikwisha tabiri uchaguzi wa Marekani kuwa Bi. Hillary Clinton atashinda lakini matokeo yakawa tofauti na utabiri pamoja na uchaguzi wa Tanzania alikosea kutabiri ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika 2015.
Aidha Lusekelo amezidi kupigilia msumari huo kwa kudai kuwa TB Joshua hana unabii unaosomwa kwenye biblia kama kina nabii Elisha, Eliya na wengineo ambao walikuwa na uwezo wa kuona vita au maadui kabla hata hawajakaribia katika maeneo ya ufalme.
"Yule ni tapeli kwa sababu nchini kwake kuna wale mabinti waliotekwa kipindi kile mpaka leo ameshindwa kuwakomboa sasa mtu kama huyo unamuamini vipi? si mliona alimtabiria yule mama Hillary atakuwa Rais lakini akakosea hata hapa nchini si alitabiria watu watano watakuwa marais katika hali ya kawaida nchi itaongozwaje na marais wote hao ?" alihoji Mzee wa upako
Lusekelo aliongeza pia kuwa siyo kila mtu anaweza kuwa nabii huku (bila kuziweka hadharani) akisema unabii unahatua zake na sifa zake ambazo TB Joshua hana na ndiyo maana alishindwa hata kuona kuwa jengo la kanisa lake linaelekea kuanguka na badala yake akaacha watu wakapoteza maisha huku yeye akienda Afrika Kusini.