Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni mtoto wa rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete ameeleza uhusiano uliopo kati ya baba yake na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa bado ni maswahiba.
Ridhiwani ametoa ufafanuzi huo kutokana na imani iliyojengeka kuwa kuna uhasama kati ya Dkt. Kikwete na Lowassa ambao awali walikuwa maswahiba wakubwa kabla ya siasa kuingiza doa kwenye uhusiano huo.
Uhasama huo uliaminika kuwepo na kuongezeka hasa baada ya Dkt. Kikwete kuongoza kamati ya maadili ya CCM iliyoliondoa jina la Lowassa katika orodha ya waliokuwa wakiwania nafasi ya kugombea urais, hali iliyopelekea mwanasiasa huyo kuhamia Chadema na kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza wikendi hii na mtangazaji wa Clouds FM, Millard Ayo baada ya kuenea mitandaoni picha inayomuonesha akisalimiana na kuteta na Lowassa, Ridhiwani alieleza kuwa hakuna uhasama kati ya baba yake na mwanasiasa huyo mkongwe kama wengi wanavyoamini.
Aliongeza kuwa amewahi kuwashuhudia wakizungumza na kuwasiliana kama kawaida kwa njia ya simu mara kadhaa.
“Kwanza hakuna ugomvi kati ya watu hawa wawili. Unajua watu wanashindwa kuelewa kwamba hakuna urafiki katika masuala ya kazi. Kwa mfano suala lile la kumtafuta rais, jambo la kutafuta rais sio jambo la Jakaya peke yake,” alisema Ridhiwani.
“Ukweli wa mambo ni kwamba Bwana Lowassa na bwana Kikwete ni watu wanaosaidiana katika mambo mengi sana,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Ridhiwani alieleza kuwa baba yake alipoona picha yake na Lowassa wakisalimiana baada ya kukutana Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa kwenye mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga alimpigia simu kutoka Ethiopia na kumtaka kuendelea na hali hiyo kwani siasa sio vita.
“Kwa mfano hata jana jioni alinipigia simu, of course alikuwa yuko Ethiopia, akaniambia ‘bwana nimeona kwenye picha uko na bwana Edward [Lowassa] ilikuwa wapi hapo?’, nikamwambia nimekutana nae uwanja wa Taifa tulikuwa tunaangalia mpira,” “[Akasema] ‘aah naye alikuja kuangalia mpira’ nikasema ndio. Akasema ‘okay hayo ndio mambo mnayotakiwa kufanya, msifike sehemu mkaona kama siasa ni vita’.
“Kwahiyo ndio maana mimi baada ya kuongea naye akaniambia siasa sio vita, na mimi niliposhika simu yangu Instagram yangu nikaandika kwamba ‘tunaendelea kujifunza…. Lakini basically najifunza kutoka kwa maneno ya mzee wangu ambaye ameniambia kwamba ‘siasa sio vita na kwamba na ninyi katika umri wenu inabidi muendelee kujifunza’ kwahiyo hata mimi comment yangu kwenye Instagram, actually sababu yake kubwa ni hiyo,” alifafanua.
Ridhiwani alieleza kuwa alimuona Lowassa baada ya kipindi kirefu kupita hivyo aliamua kumfuata na kumsalimia ambapo pamoja na mambo mengine, Lowassa alimuuliza alipo Dkt. Kikwete na akampa salamu zake amfikishie na familia kwa ujumla.
Lowassa alilazimika kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008 katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa inaongozwa na Dkt. Kikwete kutokana na sakata la Richmond.