Shirika la Kijasusi Marekani Lafichua Mazito Juu ya Mbio za Urais Tanzania Kipindi cha Mwl Nyerere..!!!


MAREKANI ilikuwa inasumbuka kuhusu mrithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kama Rais wa Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) nani angemrithi Mwalimu Nyerere lilikuwa ni suala ambalo liliumiza vichwa vya taifa hilo tajiri duniani.

Kwa kawaida, CIA imekuwa na utaratibu wa kuweka hadharani baadhi ya siri kuhusu ujasusi wake katika mataifa mbalimbali duniani; lakini baada ya kipindi fulani kupita.

Safari hii, CIA imeweka hadharani siri za namna ilivyofuatilia matukio mbalimbali katika siasa za kitaifa za Tanzania; hususani mwelekeo wake endapo Nyerere angeondoka madarakani au angeendelea.

Kwa kawaida, ripoti hizo za CIA huwa zina ukweli  ingawa wakati mwingine –hasa kwa taarifa hizi mpya za Tanzania, kuna maeneo ambako ubashiri wao unakuwa si wa kweli na upungufu mwingine katika usahihi wa majina ya wahusika.

Musoma Group

Taarifa hizi mpya za kijasusi, zinaonyesha kwamba kuelekea mwaka 1985 ambako Uchaguzi Mkuu ulikuwa umepangwa kufanyika, kulikuwa na hali tete kuhusu mwelekeo wa taifa.

Kwanza, nchi ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi baada ya kumalizika kwa Vita ya Kagera na ilikuwa haieleweki kama Mwalimu ataendelea na urais au atamwachia mtu mwingine.

Ripoti hiyo ya kikachero ya CIA; shirika kubwa zaidi la ujasusi duniani, ilibainisha kwamba kulikuwa na kundi lililojiita Musoma Group lililoanzishwa kwa minajili ya kumbembeleza Mwalimu asiachie madaraka.

“Kundi hili lilikuwa na watu watatu mashuhuri ambao ushawishi na nguvu yao ya kiutawala ilitegemea sana kuendelea kuwapo kwa Mwalimu Nyerere madarakani.

 “Watu hao walikuwa ni Joseph Butiku aliyekuwa Katibu wa Mwalimu, Timothy Apiyo aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri na Jenerali David Musuguri aliyekuwa Mkuu wa Majeshi.

“Hawa walianzisha kundi hili kwa lengo la kumshawishi Mwalimu asiachie urais. Wao walikuwa wakimshawishi aendelee kwa sababu nguvu yao ilimtegemea zaidi yeye,” inadai sehemu ya ripoti hiyo.

Wahafidhina Vs Mrengo wa Kati

Ripoti hiyo ya aina yake, inadai pia kuhusu kuwapo kwa makundi mawili kinzani ndani ya serikali katika siku za mwisho za urais wa Mwalimu.

Kulikuwa na kundi la wanasiasa wenye mrengo wa kihafidhina walioamini kwamba Tanzania inaweza kuendelea kwa kufuata sera zake zilezile ilizokuwa nazo tangu Uhuru.

CIA inadai kwamba kundi hili liliongozwa na Profesa Kighoma Ali Malima (marehemu) na lilikuwa linaundwa na viongozi kama vile aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Charles Nyirabu, Msaidizi Binafsi wa Mwalimu, Joan Wickens (raia wa Uingereza), Butiku na Kingunge Ngombale Mwiru.

Kundi hili lilikuwa katika misuguano ya mara kwa mara na kundi la waumini wa siasa za mrengo wa kiliberali wanaodaiwa kuongozwa na Cleopa Msuya.

Ripoti hiyo inawataja wanachama maarufu wa kundi hili kuwa ni aliyekuwa Katibu Mkuu Hazina, Fulgence Kazaura, aliyekuwa Mkurugenzi  wa Benki ya NBC, Amon Nsekela, George Mbowe na Profesa Simon Mbilinyi.

Wakati wahafidhina walikuwa wakishikilia msimamo ambao uliendana na ule wa Mwalimu, waliberali walitaka serikali ikubaliane na mapendekezo ya mashirika ya fedha ya kimataifa na wahisani ili ikopesheke na kuweza kufufua uchumi wake.

Dk. Salim na Ali Hassan Mwinyi 

Nyaraka hizo za siri za CIA ambazo safari hii zimetolewa kwa amri ya Mahakama moja ya Marekani, kwa undani pia zimeeleza kuhusu wanasiasa wawili waliokuwa wakipewa nafasi ya kumrithi Nyerere endapo angekuwa tayari kuachia ngazi.

Wanasiasa waliotajwa ni aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, 1984, Dk. Salim Ahmed Salim.

Ripoti za CIA zinadai kwamba Nyerere angependa mmoja wa wawili hao awe mrithi wake – Mwinyi akifanikiwa kupata nafasi hiyo hatimaye, lakini wote walikuwa na masuala ambayo yalimpa Mwalimu shaka.

“ Salim alikuwa na uzoefu mkubwa katika medani ya kimataifa kwani alitoka kuhudumu nje ya nchi. Tatizo lake ni kwamba hakuwa na mizizi katika siasa za Tanzania kwani kufikia wakati huo alikuwa ametumia maisha yake yote ya utumishi nje ya nchi.

 “Kwa kumpitisha Salim, Nyerere hakuwa na uhakika kama watu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyombo vya ulinzi na usalama wangemkubalia –hasa ukizingatia nchi ilikuwa ikipita katika kipindi kigumu kiuchumi.

“Kwa upande mwingine, Mwinyi naye hakuwa na ushawishi mkubwa Tanzania Bara lakini kwa Mwalimu alionekana kama ni mtu ambaye asingeweza kufanya mabadiliko makubwa katika sera zilizokuwapo wakati huo,” inaeleza ripoti hiyo ya CIA kuhusu Tanzania ya mwaka 1984.

Pamoja na maelezo haya ya CIA, mahojiano yaliyowahi kufanywa huko nyuma na gazeti hili kuhusu mchakato wa kumpata mrithi wa Nyerere ndani ya CCM yana maelezo tofauti kuhusu suala hilo.

Kwa mfano, wanahistoria kama Joseph Mihangwa ambaye pia ni mwanasafu wa Raia Mwema, amewahi kueleza kwa kina kuhusu nini hasa kilitokea wakati.

Kwa maelezo yake, Nyerere alikuwa amemuandaa Edward Moringe Sokoine kuwa mrithi wake lakini kifo cha Waziri Mkuu wake huyo kilivuruga mpango wake huo.

Mihangwa pia anadai kwamba Salim ndiye aliyekuwa chaguo la Mwalimu lakini fitna na ubaguzi katika siasa za Zanzibar ndizo hatimaye zilizompa ushindi Mwinyi.

 “Kulikuwa na makundi mawili kuelekea uchaguzi wa kumpata mrithi wa Nyerere. Kundi la kwanza ni la vijana waliokuwa wakifahamika kama Young Turks waliokuwa wakimuunga mkono Salim.

 “Kundi la pili lilikuwa linaundwa na wahafidhina wa Mapinduzi ya Zanzibar ambao walimhusisha Salim na chama cha Hizbu kilichohusishwa na mauaji ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abeid Amani Karume.

 “Kundi hili la pili lilifanya kampeni kali dhidi ya Salim huku likiungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa NEC kutoka Tanzania Bara. Hivi ndivyo namna Mwinyi alivyoshinda,” aliandika Mihangwa.

Mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Getrude Mongella, anayetajwa kuwa katika kundi hili la wahafidhina, aliwahi kuzungumza na gazeti hili pia na kusema ingawa Mwalimu alijulikana kumpenda Salim, hakutumia mamlaka yake kuzuia walio wengi kumpitisha Mwinyi.

Ugumu wa Mwalimu Nyerere

Katika mambo ambayo nyaraka hizo za CIA zimeeleza kwa kina ni namna Marekani ilivyokuwa ikihofia ushawishi wa Nyerere katika siasa za Tanzania na dunia kwa ujumla.

Kwanza, CIA iliripoti kwa mamlaka za juu kuwa Nyerere, hata katika kipindi hicho cha matatizo nyumbani kwake, alikuwa na heshima kubwa katika medani ya kimataifa, kiasi kwamba mwaka huo wa 1984, alikuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa na wenzake kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

CIA ilimtaja pia Nyerere kama mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) na medani ya kimataifa kwa ujumla.

Nyaraka hizi zimeonyesha namna Nyerere alivyokuwa mwiba kwa Wamarekani; ripoti ikidai alikuwa akiishambulia Marekani kila alipopata fursa, ingawa pia imekiri kuwa Baba wa Taifa alikuwa mwiba pia kwa Urusi ya zamani.

Ripoti hiyo imetoa mfano wa mashambulizi makali ya maneno aliyoyatoa Mwalimu kwa Urusi, baada ya kuwa imeivamia kijeshi nchi ya Afghanistan.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad