KATIKA kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya, Shirika la Posta Tanzania (TPC), linasimika mfumo wa kisasa utakaogharimu Sh. Milioni 200 wa kudhibiti usalama na kurahisisha utambuzi wa vitu na matukio hatarishi na haramu yanayopitishwa au kujitokeza kupitia mtandao wa shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dk Haruni Kondo amesema leo alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam. Dk Kondo alisema mfumo huo unajumuisha ufungaji wa kamera za kiusalama (CCTV), katika Posta Kuu ya Dar es Salaam, na tayari mzabuni aliyeusimika ameshakamilisha kazi yake na ataukabidhi kwa shirika wiki ijayo. Utazinduliwa rasmi wakati wowote kuanzia hapo.
"Aidha tumesimika mifumo ya kisasa ya kiusalama ikiwa ni pamoja na mashine za ukaguzi wa mizigo katika ofisi zenye uwezekano wa kuwa uchochoro wa uhalifu wa aina hii ikiwa ni pamoja na ofisi za Zanzibar, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha," amesema.
Amesema hatua hizo zimechukuliwa na shirika ili kuhakikisha linashiriki na kuchangia kikamilifu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na usafirishaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, usafirishaji na utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi, udaganyifu katika utambulisho pamoja na uhalifu mwingine wa kimtandao wa kitaifa na kimataifa.
Mwenyekiti huyo alisema Bodi ya Wakurugenzi ya shirika imedhamiria kuongeza msukumo wa kasi ya usimamizi ili kupambana na uhalifu huo ambao una madhara makubwa kwa jamii.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa matukio ya uhalifu uliopangwa yamekuwa ni changamoto kubwa kwa mashirika ya Posta duniani.
Ametaja vitu visivyoruhusiwa kusafirishwa katika mtandao wa Posta kwa mujibu wa sheria kuwa ni pamoja na dawa za kulevya, bidhaa za kemikali zenye sumu, silaha za moto na milipuko, wanyama hai, nyara za serikali, vifaa vya mionzi, vyakula vinavyooza, betri za aina mbalimbali, vimiminika, fedha haramu, utakatishaji wa fedha na vitu vyovyote hatarishi.
Shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usimamizi wa sheria, kwa hivi sasa limeimarisha uhakiki wa mifumo yake na pia ukaguzi wa barua, vifurushi, vipeto na mizigo ili kujiridhisha juu ya usalama na uzingatiaji wa sheria.