Wakati Yanga ikikwea pipa kesho kwenda Comoro kuikabili timu ya Ngaya Club de Mbe katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, watani zao Simba watakuwa kwenye dimba la Taifa jijini hapa kusaka poiti tatu.
Simba ina pointi 48 ikiwa nyuma ya Yanga kwa pointi moja na Yanga na ushindi wowote itakaoupata kwenye dimba hilo dhidi ya Prisons ya Mbeya itakuwa na maana kwamba inarejea kwenye usukani wa ligi.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika michezo mitano ya karibuni baina ya Simba na Prisons, Wekundu wa Msimbazi wameshinda miwili wakati maafande hao wakishinda miwili huku mchezo mmoja timu hizo zikitoka sare.
Utamu wa mechi hiyo ni ushindani uliopo baina ya mabeki wa Simba chini ya mkongwe Method Mwanjali na Novaty Lufunga dhidi ya washambuliaji Prisons, Victor Hangay na Lambart Subiyanka.
Kocha wa msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ametambia ushindi walioupata dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo uliopita wa mabao 3-0 kuwa umewaongezea ari ya kuiua Prisons.
Naye Kocha wa Prisons, Abdallah Mohammed amesisitiza kwamba licha ya mchezo kuwa mgumu, lakini ushindi ndiyo matarajio yao.