Spika wa bunge la Uingereza John Bercow amepinga hatua ya Rais Donald Trump kuhutubia bunge la taifa hilo wakati wa ziara yake.
Hii ni kwa madai kwamba matamshi yake yamesababisha chuki huku mbunge mmoja akisema kuwa hayafai huku wengine wakidai hafai kupendelea upande mmoja.
Bercow alisema pingamizi dhidi ya ''ubaguzi wa rangi na ule wa kijinsia'' zinapaswa kuangaziwa sana na wanachama wa bunge hilo.
Akizungumza bungeni siku ya jumatatu, Bercow alisema kuwa anapinga Rais Trump kuhutubia mabunge yote kama ilivyo ada na viongozi wengine wa kimataifa na kuongeza kusema kuwa kulihutubia bunge sio haki bali ni heshima anayopewa kiongozi wa kimataifa.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC wa maswala ya kisiasa Eleanor Garnier, hilo ni pigo la kidiplomasia kwamba rais Trump hataruhusiwa kuhutubia bunge la nchi hiyo.