BINTI ana miaka 19, hajiwezi kutokana na udhaifu wa mwili wake. Hawezi kutembea bila msaada wa watu angalau wawili, lakini baba yake aliona ndiye anayemfaa kukidhi tamaa zake za kimwili.
Kwa miaka miwili, mkazi wa Kijiji cha Kiwanja katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Lyimo Pesambili amekuwa akimwingilia kimwili binti yake wa kumzaa, bila ya kujali udhaifu wa afya ya mtoto wake huyo.
Pesambili pia anafahamika kwa majina ya Maneno Pesambili Kanjanja ambayo aliyatumia wakati akiishi katika Kijiji cha Chalangwa wilayani humo. Bado haijafahamika sababu za mtuhumiwa huyo kutumia majina tofauti kwa maeneo tofauti aliyoishi.
Binti huyo, ambaye hata hivyo tunahifadhi jina lake, amekiri kufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili na mzazi wake. Pamoja na kukiri kuingiliwa kimwili na baba yake, binti huyo alifichua zaidi ukatili wa baba yake huyo ikiwemo kunyimwa chakula, mavazi na huduma zingine muhimu.
Ukatili dhidi ya binti huyo, ambaye kwa miaka yote miwili alifungiwa ndani, ulifahamika wiki mbili zilizopita baada ya kuonekana njiani na baadhi ya kina mama, majira ya saa moja usiku akitambaa kueleke kwenye moja ya majengo kijijini hapo.
“Jumapili ilikuwa mara ya tatu kumuona, nilipomuliza ndipo akanieleza analala kwenye ofisi za CCM, nikaita watu kupata msaada,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Maria Mwasaga, aliyemuokota binti huyo.
Pesambili hivi sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Chunya, akituhumiwa kumbaka binti yake huyo.
Alifikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha wilaya hiyo mjini Chunya Jumatatu ya Januari 23, mwaka huu baada ya kina mama kijijii hapo kuulazimisha uongozi wa kijiji kuchukua hatua.
Hata hivyo, katika maelezo ya awali yaliyoandikishwa kituo cha polisi, mtuhumiwa huyo aliandikiwa kosa la kushindwa kulea familia na sio kubaka.
Kina mama katika Kijiji hicho cha Kiwanja ndio walioingilia kati kwa kuulazimisha uongozi wa kijiji hicho kumchukulia hatua za kisheria mzazi huyo.
Hata hivyo, kina mama hao waliwaambia waandishi wa habari waliofika kijijini hapo kuwa, mazingira waliyoyashuhudia katika kituo cha polisi, yaliwapa mashaka iwapo haki ingetendeka.
Wanasema walibaini suala hilo kutopewa umuhimu na viongozi wa kijiji pamoja na polisi, wakaamua kuvijulisha baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo wa Raia Mwema ambao kufika kwao kijijini hapo mwishoni mwa Juma lililopita kuliibua njama za kulifunika jambo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa aliwaeleza waandishi wa habari waliofuatilia suala hilo kuwa hakuwa na taarifa zozote na kuelezea kushangazwa kwake kwa suala hilo kutokuwemo kwenye taarifa za polisi anazopatiwa kila siku asubuhi.
“Ndio nasikia kutoka kwenu, huu ni zaidi ya ukatili,” alisema Mkuu huyo wa wilaya katika mahojiano yake na waandishi wahabari ofisini kwake.
Binti asimulia:
Mama yake alifariki akiwa bado mtoto mdogo, alimwacha akinyonya, hivyo takribani maisha yake yote ameishi na baba yake huyo, mtuhumiwa wa ubakaji.
Binti anasimulia kuwa baba yake alikuwa na kawaida ya kumfuata anapolala baada ya kuhakikisha kuwa wadogo zake wamelala. Alimwingilia kwa nguvu, kutokana na udhaifu aliokuwa nao, hakuwa na uwezo wa kujitetea.
Mazingira ya malazi ya familia hiyo yanatisha, ni chumba kikubwa chenye kitanda kimoja ukutani kinachotumiwa na baba huku watoto wakilala kwenye sakafu bila kuwepo godoro na kikinuka uvundo.
“Akiona watoto wamelala alikwenda mlangoni, aligonga mlango kama vile mtu yupo nje anataka kuingia ndani, kisha akaja kwangu na kuniingilia,” anasimulia binti huyo katika mahojiano yake na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo.
Kwa mujibu wa binti huyo, baba yao amekuwa akimfanyia ukatili tangu akiwa bado mdogo ambapo mwaka 1998 alilazimika kukatisha masomo yake akiwa darasa la sita kwa kukosa huduma muhimu.
Manyanyaso yalimlazimisha kuacha masomo, alilazimika kufanya vibarua na biashara ndogo ndogo ikiwemo kuuza kuni ili apate fedha kwa ajili ya mahitaji yake ya shule, nguo na chakula.
“Huna mikono,” lilikuwa swali la Pesambili kwa binti yake huyo kila alipomuomba mahitaji, anasema binti huyo.
Anasema baada ya kuacha masomo, aliondoka nyumbani na kuanza kuhangaika kujitafutia maisha ikiwemo kufanya kazi kwenye machimbo ya dhahabu wilayani humo. Akiwa kwenye hizo harakati zake za kutafuta maisha ndipo alipokutana na mwanaume ambaye baadaye alikuja kuishi naye kama mumewe.
Hata hivyo, binti huyo anasimulia kuwa aliishi na mumewe kwa miaka mitatu tu kabla ya kurudishwa nyumbani kwao kutokana na kuugua ambapo alijikuta mwili ukiishiwa nguvu.
Alirudishwa kwa baba yake miaka miwili iliyopita na tangu wakati huo, alimgeuza kuwa mke wake kwa kumuingilia kimwili hata bila ya ridhaa ya binti yake ambaye tayari alikuwa mgonjwa na dhaifu.
Pesambili aliishi peke yake na watoto wake watatu baada ya mke wake, aliyeoa baada ya kufiwa na mke wa kwanza kufariki, kuondoka. Na mke uyo aliondoka kielezwa kuwa alichoshwa na mateso ya mumewe huyo.
Pamoja na mchezo wake huo mchafu kwa binti yake, bado aliendelea kutompatia huduma za muhimu ikiwemo chakula, malazi, mavazi na hata maji, ikizingatiwa kuwa hakuwa na uwezo wa kubeba vitu.
“Nilikuwa nanawa mikojo yangu, akaniambia nanuka, sina soko,” anasimulia binti huyo.
Mkazi wa Kijiji cha Kiwanja, Tunu Kitaba anasema, wao wakiwa wanawake, tukio hilo limewaumiza ndio maana waliamua kulisimamia hadi waone haki ikitendeka.
“Mwenyekiti wa kijiji alilifahamu tatizo lakini hakuchukua hatua yoyote, ndio maana tumewaita mtusaidie,” alisema Tunu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiwanja, Gideon Kinyamagoha alithibitisha kufahamu binti huyo kufungiwa ndani na kwamba alilazimika kuiagiza Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Serikali ya Kijiji hicho kufuatilia.
“Maelezo ya binti kwa kina mama, alisema baba yake alikuwa akimwingilia kimwili,” alisema Mwenyeiti huyo katika maelezo yake kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Rehema Madusa.
Polisi, ustawi wa jamii wajichanganya:
Tayari serikali wilayani Chunya imechukua hatua kuhakikisha haki inatendeka. Baada ya mahojiano yake na waandishi wa habari, mkuu wa wilaya hiyo aliamua kulifuatilia mwenyewe siku hiyo hiyo kwa kuwaita Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Chunya na Asifa Ustawi wa Jamii wa wilaya hiyo.
Ofisa Upelelezi wa Wilaya hiyo, Mkoma alibainisha kuwa kesi iliyopo kituoni hapo kuhusu Pesambili inahusu kushindwa kulea familia, kwamba wakati wa kutoa maelezo, suala la ubakiji halikutajwa.
Afisa Usatawi wa Jamii Wilaya ya Chunya, Theresia Mwendapole naye alithibitisha tatizo la binti huyo kufahamika na ofisi yake.
“Huyo baba aliwahi kuja ofisini kwangu, kuomba iwapo serikali inatoa msaada kwa watoto kama hawa waliopooza,” alisema Theresia akithibitisha kulifahamu tatizo hilo.
Theresia pia alithibitisha suala la Pesambili kumbaka binti yake huyo lilitajwa wakati wa kutoa maelezo Kituo Kikuu cha Polisi wilayani humo. Hata hivyo afisa huyo alidai kuwa suala la ubakiji lilitajwa baada ya zoezi la utoaji maelezo kukamilika.
Kwa mujibu wa Theresia, wanapokea wastani wa tukio moja la ubakaji kila wiki wilayani humo. Anasema kuwa wenyeji huvihusisha zaidi vitendo hivyo na imani za kishirikina kwa wachimbaji wa madini ya dhahabu.
Kutokana na mkanganyiko huo wa maelezo ya maafisa wa serikali, Mkuu wa Wilaya aliamua wote, yeye mwenyewe, afisa usatawi wa jamii na afisa upelelezi kwenda kijijini hapo, umbali usiozidi kilometa tano kutoka ofisi za mkuu wa wilaya.
Katika hatua ya kushangaza, tangu wananchi hao wafikishe malalamiko yao polisi na ujirani uliopo, hakuna aliyethubutu kufika kijijini hapo kujionea hali halisi.
Mkuu wa wilaya na ujumbe wake huo walikutana na uongozi wa kijiji, wananchi, kujionea makazi ya mtuhumiwa pamoja na kuonana na binti mwenye.
Mkuu wa Wilaya alimwagiza Afisa Ustawi wa Jamii kusimamia zoezi la uchunguzi wa afya kwa binti na wadogo zake.
Vile vile alimwagiza afisa upelelezi kuandika maeleo sahihi ya suala hilo na kesi isomeke ubakaji na taratibu za kisheria ziendelee ikiwemo mtuhumiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Kina mama kijijini hapo wameweka msimamo wao kwamba hawataki kumuona tena Pesambili kijijini hapo na iwapo ataachiwa na kurudi kijijini basi watajua wao cha kufanya.
Binti huyo hivi sasa anatunzwa na kina mama wa kijiji hicho akiishi kwa mmoja wao, Tunu. Kina mama hao wanaamini kuwa akipata huduma atarudi katika hali yake ya kawaida.