MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe, ameunda kamati ya watu watano kusaka mwafaka wa matumizi ya Sh bilioni 5.8 za uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) sambamba na mkakati wa kudumu wa kumaliza tatizo la usafiri Dar es Salaam.
Kamati hiyo iliundwa baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na mameya, naibu mameya wa Jiji hilo pamoja na viongozi waandamizi wa vyama vinavyounda Ukawa, kilichofanyika kwenye ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
“Tulikutana si kujadili kiasi hicho cha fedha pekee, bali kutazama wajibu wa mamlaka ya Jiji la Dar es Salaam kuwa waangalizi namba moja wa mifumo ya usafiri na haki za abiria jijini humo,” alisema Mbowe.
Alitaja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia na Naibu Meya wa Ilala.
Hivi karibuni kuliibuka mvutano kati ya Serikali na uongozi wa Jiji hilo linaloongozwa na Ukawa kuhusu kuidhinisha mabilioni hayo ya uuzwaji wa hisa asilimia 51 kati ya 100 kwa kampuni ya Simon Group.
Jumamosi iliyopita, Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo chini ya Mwita kwenye kikao chake cha kawaida lilishindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa kilichoelezwa kuwa ni sawa na kubariki ufisadi wa uuzwaji wa hisa hizo ambazo wanaona ni kiasi kidogo.
Kikao hicho kilifanyika kutokana na agizo la Rais John Magufuli Januari 27 wakati akizindua mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Katika agizo hilo Rais alitoa siku tano kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinapangiwa matumizi.
“Tumelitazama hili kwa upana na kwa kina zaidi, tumekubaliana kuunda kamati ya watu watano ambayo itakuwa ikiripoti kwangu, itakwenda kuandaa mpango mkakati wa namna ya kuboresha usafiri wa Dar es Salaam,” alisema Mbowe.
“Mapendekezo ya kamati yakikamilika ndani ya wiki moja au mbili, tutayawasilisha serikalini na imani yetu watayapokea kwani Dar es Salaam ni ya wote, leo inaongozwa na Ukawa sijui kesho itaongozwa na nani. Tunapaswa kuweka kando siasa na kutanguliza maslahi ya Taifa.”