Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema dawa za kulevya zinateketeza nguvukazi ya Taifa, jambo ambalo halipaswi kuachwa liendelee kumea.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Sheikh Alhad amesema baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya nchini linaunga mkono juhudi zifanywazo na Serikali kupambana na jambo hilo.
“Suala la matumizi ya dawa za kulevya limekuwa kikwazo cha maendeleo nchini kutokana na nguvu kubwa ya Taifa ambayo ni vijana kujihusisha na utumiaji wa dawa hizo,” amesema.
Amesema kuwa wanawataka viongozi wengine wa umma kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wa kupambana na uovu wa uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambao ni janga kwa Taifa.
“Tunawaomba wananchi wote kuunga mkono suala hili pamoja na kuonyesha ushirikiano wa kutosha kwa wale walioamua kujitoa kwa ajili ya nchi yetu.”
Katibu wa baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya nchini, Padri John Solomoni ameitaka Serikali kushughulikia suala hilo kwa umakini ili lisiibue manung’uniko miongoni mwa wananchi ambao hawana hatia.
Padri huyo amewataka viongozi wanaochunguza suala hilo kuwa makini ili wasiharibu haki ya mtuhumiwa.
“Ikumbukwe kwamba wanaotajwa ni watuhumiwa, huenda baada ya uchunguzi wakabainika kuwa hawakuhusika. Baada ya kugundulika kuwa hawana hatia na itakuwa vigumu kurudisha waliyokuwa nayo hapo mwanzoni,” amesema.
Kwa takriban wiki moja sasa, watu mbalimbali wamehojiwa na polisi kuhusiana na ama utumiaji wa dawa hizo au uuzaji katika vita inayoendeshwa na mkuu wa mkoa huo.