Waumini watano wanaotambulika chini ya mwamvuli wa imani ya Voodoo nchini Benin wamefariki dunia baada ya kuamuliwa kukaa kwenye chumba maalumu na kufanya maombi wakisubiri mwisho wa dunia.
Waumini hao waliamulia kukaa kwenye chumba kilichozibwa sehemu zote kama sehemu ya kudhihirisha imani yao.
Vifo hivyo vilisababishwa na msongamano pamoja na ukosefu wa hewa.
Waumini wengine walionusurika kwenye tukio hilo lililotokea katika Mji wa Adjarra uliopo karibu na Bandari ya Novo, Kaskazini mashariki mwa Benin wamelazwa hospitali.
Mmoja wa walionusurika kwenye tukio hilo alisema waliamuliwa kuingia kwenye chumba cha maombi ili kujisalimisha na adhabu yoyote iwapo dunia ingefikia mwisho wake.
“Tukiwa katika chumba cha maombi tulitumia nguo zilizochakaa kuziba maeneo yote yaliyokuwa wazi na baadaye kutayarisha mkaa ambao ulikuwa kama maandalizi ya kurejea kwa roho mtakatifu,” alisema Yves Aboua akiwa amelazwa katika hospitali ya Porto Novo.
Tukio hilo linakumbusha lile lililotekea nchini Uganda wakati wafuasi wa mtu aliyejiita nabii maarufu kwa jina la Kibwetele walipojitekeza kwa moto wakiamini kuwa mwaka 2000 ulikuwa mwisho wa dunia.
Baada ya tukio hilo iliripotiwa kuwa makumi ya watu walipoteza maisha ndani ya kanisa la Kibwetere.
Kwa muda sasa umekuwapo upinzani mkubwa unaojitokeza kukemea mwenendo unaofanywa na waumini wa Voodoo ambao wanalalamikiwa kwenda kinyume na misingi halisi ya imani.
Moja ya kanisa lililojitokeza wazi kukema imani hiyo ni lile linalojulikana kama Kanisa Takatifu la Yesu Kristo wa Baname.
Nchini Benin, Voodoo ni utamaduni unaotambuliwa na wengi na kuna siku maalumu ya kitaifa inayotambulika kwa jina hilo. Pia, kuna makumbusho ya Taifa ya Voodoo.