Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wa saratani wanaokadiriwa kufikia milioni 14.1, na kati ya hao zaidi ya wagonjwa milioni 8.2 hufariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika za Kimataifa la Atomiki la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani ambazo zimetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ikiwa kesho ni siku ya Saratani Duniani na kusema kuwa kwa Tanzania tatizo la saratani limekuwa likiongezeka na kukua kila mwaka.
Amesema nchini Tanzania kila mwaka wagonjwa wapya wapatao 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali na kati ya hao ni wagonjwa 5,000 sawa na asilimia 10 ya wagonjwa wote ndiyo wanaofanikiwa kufika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kuweza kupata tiba, huku asilimia 70 ya wagonjwa wanaobahatika kufika katika taasisi hiyo na kupata huduma za tiba hufika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Amesema tayari serikali imetoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ununuzi wa mashine mpya za mionzi ambazo zitasaidia kutibu wagonjwa wa saratani.